Shinikizo lazidi dhidi ya rais wa FIFA Blatter
28 Mei 2015Rais wa FIFA Sepp Blatter, amesalia faraghani wakati vichwa vya habari vya kimataifa vikilikashifu shirikisho hilo na hata wito kutolewa wa kumtaka Mswisi huyo mwenye umri wa miaka 79 ajiuzulu. Blatter hata hivyo anaonekana kuwa atashinda uchaguzi wa urais wa FIFA hapo kesho. Andre Marty ni msemaji wa ofisi ya Mwanasheria mkuu wa Uswisi "kwa sasa, Bwana Sepp Blatter hayuko chini ya uchunguzi na siyo mmoja wa watu tutakaowahoji. Lakini ofisi ya mwanasheria mkuu haitasita kumuuliza maswali yeyote, kukiwa na haja, lakini kwa sasa hakuna haja kwa sababu Bwana Blatter ni mkaazi wa Uswisi, hivyo kinadharia tunaweza kumwalika ili atupe habari zozote alizo nazo".
Kampuni kubwa ya kadi za benki VISA imesema “itatathmini” upya ufadhili wake kwa FIFA ikiwa haitachukua hatua ya haraka baada ya maafisa wakuu wa FIFA kukamatwa wakituhumiwa na maafisa wa Marekani kwa kukula kiasi kikubwa cha hongo. Wakati polisi ya Uswisi ikichunguza kutolewa vibali vya Kombe la Dunia la mwaka wa 2018 na 2022 kwa Urusi na Qatar, nyaraka za Marekani zinaonyesha kuwa Afrika Kusini ilitoa hongo ya kiasi cha dola milioni 10 kwa maafisa wa FIFA ili kupata kibali cha kuandaa Kombe la Dunia mwaka wa 2010.
Afrika Kusini hata hivyo imetoa taarifa ikikanusha madai hayo. Kampuni za Coca-Cola, Adidas, McDonald's na Budweiser zote zimetoa kauli zao dhidi ya kashfa hiyo ya ufisadi. Mwanasheria mkuu wa Marekani Loretta Lynch ameeleza ni kwa nini maafisa hao walikamatwa. "walistahili kuheshimu sheria ambazo zinaweka uaminifu katika kandanda na kulinda uadilifu wa mchezo huo. badala yake, waliweka ufisadi katika biashara ya kandanda kote ulimwenguni kwa maslahi yao wenyewe na kujinufaisha. Wizara ya sheria imejitolea kumaliza tabia hii, kuondoa ufisadi na kuwashtaki wanaofanya uovu huu".
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa amesema itakuwa ni busara kuuchelewesha uchaguzi wa kumchaguwa rais mpya wa FIFA. Shirikisho la kandanda la Ulaya – UEFA pia limetoa wito wa kuahirishwa uchaguzi huo na unatarajiwa kukutana leo kuamua ikiwa utasusuia zoezi hilo.
Maafisa saba wa kandanda wakiwemo makamu wawili wa rais, wangali kizuizini nchini Uswisi. Maafisa wa Marekani wanasema jumla ya maafisa tisa wa kandanda ni miongoni mwa watu 14 wanaokabiliwa na hadi kipindi cha miaka 20 jela ikiwa watapatikana na hatia katika kesi hiyo iliyodumu kwa muda mrefu ya ufisadi inayohusisha hongo za zaidi ya kiasi cha dola milioni 150.
Makamu wa rais wa FIFA Jeffrey Webb ambaye ni mkuu wa sasa wa shirikisho la kandanda la CONCACAF na Eugenio Figuerdo, aliyekuwa mkuu wa shirikisho la kandanda Amerika ya Kusini, ni miongoni mwa watu saba waliokamatwa na polisi ya Zurich. Jack Warner, makamu wa rais wa zamani, alifika katika mahakama moja ya mji wa Port of Spain nchini Trinidad and Tobago jana kabla ya kuachiliwa kwa dhamana ya dola 394,000, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo. Warner anakanusha madai ya rushwa.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Josephat Charo