BERLIN : Merkel ataka kupunguzwa gesi zinazoathiri mazingira
25 Mei 2007Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amehimiza upunguzaji mkubwa wa gesi zenye kuathiri mazingira duniani.
Hata hivyo amesema kwamba hana uhakika iwapo mkutano unaokuja wa viongozi wa Kundi la Mataifa Manane G8 yenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani utatowa ufumbuzi wa vita dhidi ya kuongezeka kwa kiwango cha ujoto duniani.Merkel atakuwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi wa kundi la Mataifa Manane G8 utakaofanyika kwenye mji wa kitalii wa Heilegendamm nchini Ujerumani kuanzia tarehe sita mwezi wa Juni ambao unategemewa kulenga juu ya mabadiliko ya hali ya hewa kuendeleza ukuaji wa uchumi barani Afrika na ushirikiano wa kiuchumi duniani.
Merkel alikabiliwa na upinzani hususan kutoka Marekani katika jaribio lake la kuweka msingi kwa ajili ya kuongeza muda makubaliano ya Itifaki ya Kyoto juu ya mabadiliko ya hali ya hewa katika mkutano huu wa viongozi.