BERLIN : Hatua dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa zapita
24 Agosti 2007Serikali ya mseto ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani imekubaliana juu ya mpango wa hatua kadhaa wenye lengo la kusaidia kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mpango huo umeidhinishwa na mkutano maalum wa baraza la mawaziri wa siku mbili huko Meseberg karibu na Berlin wakati wa kuanza kwa kipindi cha pili cha miaka minne madarakani kwa serikali hiyo.
Sigmar Gabriel waziri wa mazingira nchini Ujerumani anasema lengo ni kwa kanuni za msingi za mkutano wa Umoja wa Mataifa wa hali ya hewa wa Bali uliopangwa kufanyika mwezi wa Desemba zinaweza kubadilishwa kuwa sheria kwa kuletwa kwenye bunge la Ujerumani na pia wataweka wazi kwamba misimamo hiyo ya juhudi za pamoja inawasilishwa kwenye mkutano huo.
Hatua hizo ni matokeo ya majadiliano mazito kati ya Waziri huyo wa Mazingira Sigmar Gabriel wa Chama cha Social Demokratik na Waziri wa Uchumi muhafidhina Michael Glos.
Serikali inataka kupunguza utowaji wa gesi zenye kuathiri mazingira kwa asilimia 36 ifikapo mwaka 2020 kwa kulinganisha na viwango vya mwaka 1990.