1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yaiangamiza Barca, Champions League

2 Mei 2013

Mashabiki wa Bayern Munich walisherehekea kipigo cha pili katika muda wa siku tisa dhidi ya timu ya Barcelona iliyotamba na usakataji wake wa soka katika bara la Ulaya na pengine dunia, ilipokubali kipigo cha mabao 3-0.

https://p.dw.com/p/18QJb
Bayern Munich's players celebrate their victory at the end of the UEFA Champions League semi-final second leg football match FC Barcelona vs FC Bayern Munich at the Camp Nou stadium in Barcelona on May 1, 2013. Bayern Munich won the match 3-0. AFP PHOTO / LLUIS GENE (Photo credit should read LLUIS GENE/AFP/Getty Images)
Bayern Munich wakisherehekea ushindi mnono dhidi ya BarcelonaPicha: Lluis Gene/AFP/Getty Images

Barcelona ilichezea kipigo cha mabao 4-0 mjini Munich Jumanne iliyopita na kipigo cha jana (01.05.2013), kinaashiria kuwa huenda utandazaji wa soka wa kile kinachojulikana kama " tiki taka" , unaelekea ukingoni.

Bayern Munich ilivamia ngome ya Nou Camp na kufanikiwa kupata nafasi ya kuingia katika fainali ya kwanza ya timu mbili za Ujerumani katika kinyang'anyiro cha Champions League. Bayern imekamilisha hatua hiyo kwa kipigo cha jumla ya mabao 7-0 dhidi ya barcelona, na kuingia katika daraja la kuitwa wafalme wapya wa Ulaya.

Wazee wa Tiki Taka Barcelona wakitoka uwanjani vichwa chini na mikoni viunoni
Wazee wa Tiki Taka Barcelona wakitoka uwanjani vichwa chini na mikoni viunoniPicha: Lluis Gene/AFP/Getty Images

Mabingwa hao wapya wa Bundesliga , ambao wanafukuzia ubingwa wao wa tano katika mashindano hayo ya bara la ulaya , watapambana na Borussia Dortmund hapo Mei 25 katika uwanja maarufu wa Wembley mjini London.

Messi aduwaa

Nyota wa Barcelona Leonel Messi alikuwa akitazama tu akiwa benchi wakati Bayern ilipokamilisha dhoroba yake na kuwasambaratisha mabingwa hao watarajiwa nchini Uhispania kwa mabao 3-0.

Kwa kumuweka benchi mfungaji wao huyo maarufu baada ya kupata maumivu ya paja , Barcelona walishindwa kuipa changamoto ya maana Bayern, na kushindwa kufurukuta kuweza kupindua matokeo ya hapo awali ya mabao 4-0 mjini Munich.

Bayern , kwa hiyo imeidhalilisha timu ambayo kila mmoja alikuwa akiimezea mate katika soka la Ulaya kwa mara ya pili katika kipindi cha siku tisa. "Nafikiri tulicheza vizuri sana, ni historia," mshambuliaji wa Bayern Arjen Robben amesema. "Iwapo tutaendelea kufanya kama hivi , dhidi ya timu ambayo imekuwa ikitawala soka katika bara la Ulaya katika kipindi cha miaka mitano, timu ambayo ina wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu, inashangaza." Ameongeza Robben.

epa03684152 FC Barcelona's Argentinian striker Lionel Messi sits on the bench during the UEFA Champions League semi final second leg soccer match between FC Barcelona and Bayern Munich at Camp Nou in Barcelona, Spain, 01 May 2013. EPA/ANDREU DALMAU
Leonel Messi akitumbua macho tu bila kujua la kufanyaPicha: picture-alliance/dpa

Bayern ilipima joto kwanza

Baada ya Bayern Munich kupima joto katika kipindi cha kwanza , Robben hatimaye alifungua ukurasa wa magoli katika dakika ya 49 kabla ya mlinzi wa Barcelona Gerard Pique kujifunga mwenyewe katika dakika ya 72. Thomas Muller alikamilisha karamu hiyo ya mabao kwa Bayern dakika nne kabla ya mchezo kumalizika, wakati Barcelona ikitumbukia katika kipigo chake cha kwanza nyumbani katika mashindano ya Ulaya tangu mwaka 2009.

Pique amekieleza kipigo hicho kuwa ni moja kati ya usiku mbaya kabisa katika historia ya klabu yake, na kuongeza kuwa hata kama Messi angekuwapo asingeweza kubadilisha mambo.

Bayern Munich's Rafinha, Thomas Mueller and Arjen Robben (L to R) celebrate after their Champions League semi-final second leg soccer match against Barcelona at Camp Nou stadium in Barcelona May 1, 2013. REUTERS/Gustau Nacarino (SPAIN - Tags: SPORT SOCCER)
Wachezaji wa Bayern wakipongezaja baada ya bao.Picha: Reuters

Bayern ilijiandaa

Bayern Munich ilianza kujenga msingi wa msimu huu wenye mafanikio kuelekea fainali ya Champions League mara tu baada ya kushindwa kulinyakua kombe hilo mbele ya Chelsea msimu uliopita, amesema kocha wa Bayern Jupp Heynckes.

Heynckes ameongeza kuwa maumivu waliyopata baada ya Chelsea kulinyakua kombe la Champions League nyumbani kwa Munich kwa mikwaju ya penalti , yalimuongezea motisha ya kujaribu kufanya vizuri mara hii

Kuanzia siku ya kwanza baada ya kipigo dhidi ya Chelsea , uliweza kuona kuwa kila mmoja wetu alikuwa akijitahidi kubadilisha mambo, amesema kocha huyo mzoefu , mwenye umri wa miaka 67.

Bayern inakutana na Borussia Dortmund katika fainali hapo Mei 25, lakini siku ya Jumamosi hii, kutakuwa na mpambano wa majaribio ya fainali hiyo kati ya timu hizo mbili zinazokaribiana katika mpambano wa Bundesliga.

Mwandishi: Sekione Kitojo /rtre /ape