Dortmund yafika fainali
1 Mei 2013Dortmund waliishinda Madrid kwa jumla ya magoli manne kwa matatu, baada ya ushindi wao wa magoli manne kwa moja katika mechi ya mkondo wa kwanza. Huku wakiitaji muujiza mkubwa wa kubadilisha mambo baada ya kichapo cha wiki iliyopita, Real walionekana kuishiwa kasi, baada ya Gonzlo Higuain, Cristiano Ronaldo na Mesut Ozl kupoteza nafasi za wazi katika dakika za mapema.
Hata hivyo, baada ya Robert Lewandowski kusukuma kombora safi lililogonga chuma naye kipa Diego Lopez kufanya muujiza na kulizuia kombora la karibu la Ilkay Gundogan, Madrid walipata nguvu tena katika dakika ya 83 wakati nguvu mpya Karim Benzema kubusu nyavu kutoka pasi safi iliyoandaliwa na Ozil.
Na dakika sita baadaye wakapata matumaini ya kweli ya kubadilisha matokeo hayo baada ya nahodha Sergio Ramos kusukuma bazuka ndani ya nyavu na kufanya mambo kuwa mawili bila jawabu, ila walihitaji bao la tatu ili kufuzu.
Dortmund walistahimili dakika tano za kijasho ili kujikatia tikiti ya kucheza katika fainali itakayoandaliwa kwenye uwanja wa Wembley jijini London mwezi ujao. Kocha wa Dortmund Jurgen Klopp amesema Real huenda walikuwa timu bora ya usiku, lakini hilo halikuwa na maana yoyote kwa sababu vijana wake wametimiza lengo lao la kufika fainali na kwamba amejivunia mchezo wao. Mwenzake wa Real Jose Mourinho, matokeo hayo yalimaanisha kuondolewa nje ya dimba hilo katika awamu hiyo kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Dortmund sasa ni miamba Ulaya
Klopp amesema kuwa sasa Dortmund wanapaswa kutambulika kama mojawapo ya timu mahiri za soka barani Ulaya baada ya kuwabandua nje Real Madrid. Ameongeza kuwa hawajali ni nani watakayekutana naye katika fainali, lakini kila mtu ataona kuwa hawatakwenda Wembley kama watalii bali kushinda kombe.
Klopp hata hivyo amemshutumu refarii Muingereza Howard Webb akisema kuna matukio ambayo beki wa Madrid Sergio Ramos alistahili kupewa adhabu kali, kutokana na namna alivyokuwa akimchezea kimabavu Robert Lewandowski.
Wakati Klopp akilalamika kuhusu Ramos, naye Mourinho anadai kuwa refariii alistahili kumtimua uwanjani Mats Hummels kwa kuunawa mpira katika kipindi cha pili. Matokeo hayo ya Real Madrid yameendelea kuibua maswali kuhusiana na hatima ya Mreno huyo. Mourinho amesema atasubiri hadi mwisho wa msimu ili kujadili na wasimamizi wa klabu kuhusu mkataba wake.
Mourinho amesema anafahamu kuwa anapendwa nchni England, anapendwa na mashabiki na vyombo vya habari. Anasema “ninapendwa na baadhi ya vilabu, hasa kimoja. Lakini Uhispania mambo ni tofauti, watu kadhaa wananichukia, wengi weu ndani ya chumba hiki”.
Katika mechi ya pili leo, Barcelona wanawakaribisha Bayern Munich ambao wakilenga kugeuza matokeo ya mkondo wa kwanza ya mabao manne kwa sifuri. Barcelona watastahili kufanya kazi ya ziada uwanjani Camp Nou katika kuzuia kile wengi wanaona kitakuwa ni Fainali ya timu mbili za Ujerumani uwanjani Wembley, “Der Klassiker”.
Mwandishi: Bruce Amani/AP/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman