1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bashir na Kiir wakutana Addis Ababa

Admin.WagnerD4 Januari 2013

Marais wa Sudan na Sudan kusini wanakutana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, katika juhudi za kujaribu kumaliza uhasama kati yao, na kuanzisha biashara ya mafuta inayovuka mipaka kati ya nchi hizo mbili.

https://p.dw.com/p/17DgF
Marais wa Sudan na Sudan Kusini katika mazungumzo mjini Addis Ababa
Marais wa Sudan na Sudan Kusini katika mazungumzo mjini Addis AbabaPicha: Reuters

Mkutano huu umeanza huku marais hao wawili, Omar al-Bashir wa Sudan na Salva Kiir wa Sudan Kusini wakiwa tayari wameelezea wako tayari kulegeza misimamo, ili kumaliza mkwamo juu ya kuwekwa kwa eneo lisilo na shughuli za kijeshi kwenye mpaka baina ya nchi zao, baada ya uhasama ambao ulitishia kuzipeleka nchi hizo katika vita kamili mwezi Aprili mwaka jana.

Mwezi Septemba marais hao walisaini makubaliano mjini Addis Ababa juu ya kuanzishwa upya kwa usafirishaji wa mafuta na kuondoa mvutano mpakani, lakini makubaliano hayo hayajatekelezwa kutokana na kutoaminiana kati ya nchi hizo, ambazo zilipigana vita virefu kabla ya Sudan Kusini kujipatia uhuru wake mwezi Julai, 2011.

Mapigano ya Aprili mwaka jana yalikaribia kuziingiza Sudan mbili katika vita kamili
Mapigano ya Aprili mwaka jana yalikaribia kuziingiza Sudan mbili katika vita kamiliPicha: Reuters

Uaminifu bado ni tatizo

Biashara ya mafuta inao umuhimu mkubwa kwa uchumi wa nchi hizo, na Sudan Kusini hulazimika kulipa mamilioni ya dola kwa Sudan ili kutumia mabomba yake kuyasafirisha nje mafuta yake. Wachambuzi wanasema kuwa ingawa Sudan Kusini inahitaji kuwa na ushirikiano mwema na Sudan, vile vile inapendelea mivutano na jirani huyo wa kaskazini ili kuimarisha uhalali kwa watu wake, na kuyafunika mapungufu iliyo nayo katika kuendesha uchumi, pamoja na ubadhirifu.

Mkutano wa leo mjini Addis Ababa umetokana na msukumo wa nchi za magharibi na Umoja wa Afrika, katika kujaribu kwa mara nyingine kupata muafaka.

Umoja wa Afrika utajaribu katika mkutano huu kupata makubaliano ya kumaliza mzozo wa mpakani ili kuanzishwa tena usafirishaji wa mafuta, na wanadiplomasia wana imani kwamba hilo likifanikiwa, Sudan na Sudan Kusini zitakuwa zimepata mahali pa kuanzia mazungumzo juu ya matatizo yatakayobakia, kama vile umiliki wa jimbo la Abyei, na utata wa mpaka.

Bado mpaka kati ya Sudan na Sudan Kusini unaleta utata
Bado mpaka kati ya Sudan na Sudan Kusini unaleta utata

Ari mpya ya maelewano

Alhamis shirika la habari la Sudan, SUNA, lilisema kwamba rais al-Bashir anakwenda mjini Addis Ababa kuharakisha utekelezwaji wa makubaliano ya mwezi Septemba. Naye rais Kiir wa Sudan Kusini, alieleza katika hotuba yake ya mwaka mpya, kwamba serikali yake iko tayari kuondoa wanajeshi wake mpakani.

Hata hivyo, wanadiplomasia wanatilia shaka ahadi hizo, kwa sababu nchi hizo mbili zinayo historia ya kushindwa kutimia makubaliano zilizoyatilia saini.

Jana, yaani siku moja kabla ya mkutano wa leo mjini Addis Ababa, tayari Sudan Kusini imeishutumu Sudan kufanya mashambulizi ya anga kusini ya mpaka unaozozaniwa kati yao. Jeshi la Sudan halijazijibu shutuma hizo, lakini mara kwa mara imekuwa ikizikanusha shutuma kama hizo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE

Mhariri:Josephat Charo