Hongera sana Sudan na Sudan Kusini kwa kumaliza mzozo kati yenu
28 Septemba 2012Kufuatia makubaliano hayo, Uingereza, Marekani na Umoja wa Ulaya, zote zimeipongeza hatua hiyo, huku Rais Barack Obama akisema kuwa hatimaye Sudan na Sudan Kusini sasa zitakuwa na amani. Aidha, Obama amezitaka nchi hizo kuendelea na majadiliano wakati makubaliano hayo yakitekelezwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague, naye amesema hiyo ni hatua kubwa liyofikiwa, na bila shaka itasaidia pia katika kurejesha amani baina yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sera ya Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, amesema makubaliano hayo yanawasilisha hatua ya kihistoria kwa nchi hizo ambazo awali zilikuwa hasimu.
Tutahakikisha hatupigani tena: Kiir na Bashir
Awali, Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, alisema makubaliano hayo yanakomesha machafuko yaliyodumu kwa muda mrefu baina ya nchi yake na taifa la Sudan. Rais wa Sudan, Omar al- Bashir, naye akaahidi kushirikiana na mwenzake kurejesha utulivu na usalama katika eneo hilo.
Baada ya majadiliano marefu mjini Addis Ababa, Ethiopia, yaliyoanza Jumapili iliyopita, hatimaye viongozi hao wawili walisaini makubaliano ya kushirikiana, siku moja tu baada ya muda uliopangwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa nchi hizo kutanzua tofauti zao, kumalizika.
Hatahivyo, Sudan na Sudan Kusini zimeshindwa kufikia muafaka juu ya eneo la Abyei sanjari na maeneo mengine yanayogombaniwa katika mipaka yao.
Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, amesema "Tumekuwa na machafuko katika mipaka yetu na hata nje ya mipaka hiyo. Tumekabiliwa na matatizo ya kiuchumi na tumepoteza kabisa imani ya umma tunaouongoza kutokana na utawala mbovu. Sasa serikali inafanya marekebisho katika taasisi zake ili kujenga utawala bora na kurejesha imani miongoni mwa umma."
Sudan zote mbili zaanza tena kupeleka nje mafuta
Kufuatia makubaliano hayo, sasa Sudan zote mbili zitaanza tena kupeleka mafuta nje ya nchi, mkwamo ambao umeathiri sana mapato ya mataifa hayo mawili.
Mazungumzo hayo, yaliyosimamiwa na Umoja wa Afrika, AU, yalianza mjini Addis Ababa miezi kadhaa kabla ya Sudan Kusini kujitenga mwezi Julai mwaka jana kutoka taifa la Sudan ambalo ndilo lilikuwa kubwa kabisa kuliko yote barani Afrika.
Mpatanishi mkuu wa mzozo huo, aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, amesema anaamini makubaliano baina ya Sudan na Sudan Kusini yatazaa matunda na kwamba nchi hizo mbili hazitarejea tena katika vita.
Mwandishi: Ndovie, Pendo Paul\AFP
Mhariri: Miraji Othman