Baraza la Usalama: Mataifa makubwa yakiri kukoseana imani
4 Mei 2023
Mjadala wa kujenga uaminifu kati ya mataifa umependekezwa na Uswisi ambayo ni mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Ignazio Cassis amesema kuaminiana ni kigezo muhimu katika mchakato wa kujenga amani.
Amesema wakati Umoja wa Mataifa ulipoundwa baada ya vita vikuu vya pili, jukumu lake lilikuwa kuepusha vita vingine vya dunia, na mataifa hasimu wakati huo yaliaminiana. Licha ya Umoja wa Mataifa kujitwisha jukumu hilo, amesema mwanadiplomasia huyo wa Uswisi, leo hii dunia bado inakabiliwa na vita.
Mataifa yapaswa kusikia kilio cha dunia kutaka amani
Waziri Cassis amesema diplomasia ya kimataifa inakabiliwa na shinikizo kubwa, na kuongeza kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapaswa kukiri kuwa hazitilii maanani mfadhaiko na changamoto vinavyoiandama dunia. Hata hivyo, waziri huyo wa mambo ya nje wa Uswisi amesema matumaini bado yapo.
Soma zaidi: Urusi, mataifa ya Magharibi uso kwa uso Baraza la Usalama
''Ni kweli kwamba mfumo wa kimataifa uko chini ya shinikizo, lakini matumaini hayajapotea kabisa,'' amesema na kuongeza kuwa kukaa tu bila kufanya chochote ndio kushindwa kikamilifu.
''Wakati umewadia kwa Baraza la Usalama kubeba majukumu yake, na kuchukua hatua thabiti kukabiliana na mizozo ambayo idadi yake inaongezeka kila uchao,'' amesisitiza mwanadiplomasia huyo.
Aidha, waziri Ignazio Cassis amelitaka Baraza la Usalama kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha amani na usalama duniani, na kukarabati madaraja kati ya jamii za watu yaliyovunjika.
Urusi yazilaumu ''hila za nchi za magharibi''
Kwa upande mwingine, balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia amezungumzia vizingiti vinavyokwaza maelewano baina ya mataifa wanachama wa baraza la usalama, akisema kuna pengo kubwa la imani kati ya mataifa hayo 15. Kwa maoni yake, alichokiita ''vitendo vya hila'' vya nchi za magharibi vinapaswa kulaumiwa kwa hali hii.
Soma zaidi:Ukraine yatoa wito wa kufanyika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la UN
Mwakilishi huyo wa Urusi amesema mnamo miaka 15 hadi 20 iliyopita, nchi hizo zimeng'oa hatua kwa hatua mizizi ya ushirikiano iliyoota baada ya kumalizika kwa vita baridi, akitaja kwa hali ya kipekee alichokielezea kama ''ahadi zilizovunjika'' za kutoipanua Jumuiya ya kujihami ya NATO, harakati za nchi za magharibi kuunga mkono mapinduzi upande wa Ulaya Mashariki, na dhamira ya kushinikiza mpangilio wake wa jinsi dunia inavyopaswa kuendeshwa.
Balozi wa Albania ambayo ni mwanachama wa NATO, Ferit Hoxha amekinzana na kauli hiyo ya balozi wa Urusi, akisema linachopaswa kukifanya Baraza la Usalama ni kuonyesha njia ya amani na usalama, badala ya kuchukuliwa mateka na wavamizi wanaoyumbisha usalama wa mataifa jirani, ikiwemo Urusi na uvamizi wake dhidi ya Ukraine.
Vyanzo: ape, EBU