1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama laridhia ombi la DRC kuondoa walinda amani

20 Desemba 2023

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15 jana limepiga kura na kuridhia ombi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo la kuondoa askari wa kulinda amani nchini humo kwa awamu kuanzia mwezi huu.

https://p.dw.com/p/4aMtK
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo | MONUSCO
Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MONUSCOPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Azimio hilo ambalo linaongeza mamlaka ya ujumbe wa kulinda amani nchini Kongo kwa mwaka mmoja zaidi, linajumuisha mipango ya kuondoka kwa walinda amani kutoka jimbo la Kivu Kusini kufikia mwishoni mwa mwezi Aprili.

Hatua ya kuwaondoa askari hao wa kulinda amani inatokea licha ya wasiwasi wa Umoja wa Mataifa kuhusu matukio ya ghasia katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Serikali ya Kinshasa inatoa hoja kwamba, askari hao wameshindwa kutelekeza majukumu yao ipasavyo ikiwemo kuwalinda raia dhidi ya makundi ya waasi wanaoendesha oparesheni zao katika eneo la mashariki mwa Kongo.

Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Robert Wood amesema kuwa, wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa watakuwa wanafuatilia kwa ukaribu jinsi serikali ya Kongo itakavyotelekeza jukumu lake la ulinzi wa raia wake wakati MONUSCO itakapoondoka nchini humo.