Barabara za Afrika ni hatari zaidi duniani
2 Oktoba 2024Afrika yenye barabara na magari machache zaidi katika eneo lolote duniani, lakini ni bara lenye idadi kubwa ya watu wanaokufa kutokana na ajali za barabarani.
Ajali hizo zinachochewa na uzembe, mwendo kasi, ulevi na miundombinu duni. Ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni WHO imetaja pia uchakavu wa magari na ukosefu wa waokoaji kama sababu za idadi kubwa ya vifo vya ajali za barabarani Afrika.
Jean Todt mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya usalama wa barabarani amesema kinachotia wasiwasi ni ongezeko la idadi ya vifo barani Afrika. Ongezeko hilo lilishuhudiwa katika nchi 28 kati ya 54 za bara hilo. Waathiriwa wakubwa wa ajali za barabarani ni watu wanaotembea kwa miguu, wakiwa ni theluthi moja ya jumla ya vifo kutokana na ukosefu wa barabara za kutosha.
Wataalamu wanasema maeneo mengine pia yanakabiliwa na changamoto kama hizo. Na nyingine kama za kutofunga mikanda ama kutovaa kofia ngumu.
Changamoto za uendeshaji gari Afrika
Lakini kwa Afrika ambako vifo 620 vya barabarani hutokea kila siku, hali huwa ni mbaya zaidi. Ripoti hiyo ya Shirika la WHO imesema Afrika imelitangulia eneo la Kusinimashariki mwa Asia kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo vya barabarani.
Jean Todt amesema Afrika inahitaji kuwa na barabara zilizobuniwa na kujengwa vyema, zenye alama za kutosha na njia za waenda kwa miguu, hasa karibu na shule. Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa alilaumu pia uhaba wa usafiri wa umma kwenye maeneo ya miji katika bara hilo linalokua kwa kasi.
Kampeni ya uhamasishaji
Shirika la Afya Ulimwenguni limesema hadi sasa ni nchi 13 pekee barani Afrika ambazo zimeunda mikakati ya kitaifa ya kukuza matembezi na baiskeli.
Kulingana na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Usalama Barabarani moja ya shida kubwa pia ni ubora wa magari yanaendeshwa katika barabara za Afrika. Mengi yana umri wa zaidi ya miaka 15.
Umoja wa Mataifa umetoa wito wa "muongo wa hatua" ili kupunguza nusu ya idadi ya vifo vya barabarani ifikapo 2030.