Ayatollah amuita Trump "kichekesho"
17 Januari 2020Khamenei amehutubia kwenye ibada ya swala ya Ijumaa leo hii ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minane.
Mara ya mwisho alitoa hotuba ya ibada kama hiyo, Februari 2012 wakati alipoifananisha Israel na uvimbe wa saratani huku akiapa kumuunga mkono yoyote atakayelikabili taifa hilo. Lakini pia alionya dhidi ya mashambulizi ya Marekani nchini Iran kufuatia mpango wake wa nyuklia.
Kwenye swala hii ya leo kiongozi huyo wa juu kabisa nchini Iran amesema mashambulizi ya jeshi la nchi yake dhidi ya kambi za Marekani zilizoko nchini Iraq mapema mwaka huu yalikuwa ni pigo dhidi ya Marekani inayojulikana kama taifa lenye nguvu zaidi ulimwenguni.
Khamenei amesema Marekani kwa ujinga wake ilimuua kamanda wa juu wa jeshi aliyeongoza mapambano dhidi ya kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS, Jenerali Qassem Soleiman katika shambulizi la mjini Baghdad.
Ayatollah Khameneiameshika madaraka hayo tangu mwaka 1989 na ana kauli ya mwisho kwenye maamuzi muhimu. Kiongozi huyo mwenye miaka 80 alishindwa kuzuia machozi hadharani kwenye mazishi ya Jenerali Soleimani na kuapa kulipa kisasi kikali dhidi ya Marekani.
Aidha Ayatollah amezungumzia mkataba wa nyuklia wa Iran ambao nchi hiyo ilitiliana saini na mataifa sita yenye nguvu duniani akisema mataifa matatu ya Ulaya yaliyokuwa sehemu ya mkataba huo ambao tayari Marekani imekwishajiondoa hayawezi kuaminiwa na hatua zao za kuishinikiza Iran kamwe hazitaweza kufanikiwa.
Kauli hii inakuja baada ya ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuchochea kutumika kwa mfumo rasmi wa kutatua mizozo kwenye mkataba huo hatua inayoweza kusababisha Umoja wa Mataifa kuirejeshea vikwazo Iran.
Lakini pia amewatuhumu wale aliowaita maadui wa Iran neno ambalo hulitumia zaidi anapoizungumzia Marekani pamoja na washirika wake kwa kujaribu kutumia shambulizi la bila ya kukusudia la Iran dhidi ya ndege ya Ukraine ili kufunika huzuni za watu dhidi ya kifo cha Jenerali Soleimani. "Watu wengine wanafuata na kuongozwa na Televisheni za Marekani na redio ya Kiingereza ambazo zilijaribu kuelezea tukio hili kwa njia ambayo mauaji ya mashahidi wawili Qasem Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis yatasahaulika" amesema Khamenei.
Lakini pamoja na hayo yote kiongozi huyo ametoa wito wa umoja wa kitaifa na watu kujitoa kwa wingi kushiriki uchaguzi utakofanyika mwezi Februari, baada ya maandamano yaliyoibika kufuatia jeshi kukiri kuidungua kwa bahati mbaya ndege ya Ukraine.
Amesema, ipo haja ya kuchukuliwa hatua za kuzuia ajali za bahati mbaya kama hiyo iliyosababisha vifo vya watu 176 waliokuwa ndani ya ndege.