Mataifa yaliopoteza raia ajali ya ndege ya Ukraine kukutana
13 Januari 2020Wakati huo huo, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni nchini Ujerumani amesema watu wa Iran wanapaswa kuruhusiwa kufanya maandamano ya amani na huru, baada ya maafisa nchini Iran kukiri kuiangusha ndege ya abiria ya Ukraine.
Akizungumza kandoni mwa ziara rasmi nchini Singapore leo, waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine Vadym Prystaiko amesema nchi hizo pia zitajadili kulipwa fidia na uchunguzi kuhusiana na ajali hiyo. Watu wote 176 waliokuwamo katika ndege hiyo walifariki katika ajali hiyo siku ya Jumatano, dakika chache baada ya ndege hiyo kuruka kutoka katika uwanja wa ndege wa Tehran.
Prystaiko amesema maelezo kutoka Iran kuwa ndege hiyo ya shirika la ndege la Ukraine iliangushwa wakati ikiruka karibu na eneo nyeti la kijeshi wakati wa kipindi cha wasi wasi wa hali ya juu , yalikuwa ni "upuuzi". Amesema Tehran imekubali kukabidhi visanduku vyeusi vya ndege hiyo kwa Ukraine ili kufanya uchunguzi zaidi.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas ameitaka Iran leo kuacha kuingilia kati mizozo katika eneo hilo wakati wa ziara yake nchini Jordan.
Wairani wana haki ya kuandamana
"Tumekubaliana. Iwapo Iran inataka kupunguza hali ya kuongezeka kwa wasi wasi, inapaswa kuacha uchokozi katika eneo hilo, ambalo ni pamoja na Iraq," Maas amesema hayo baada ya kukutana na mwenzake wa Jordan , Ayman Safadi.
"Wairani wana haki ya kuingia mitaani kuelezea "masikitiko yao na pia hasira zao" baada ya ajali ya ndege, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani Maria Adebahr amesema.
"Tunaamini hili linapaswa kutokea kwa amani , uhuru na bila vizuwizi."
Maandamano yalizuka mwishoni mwa juma baada ya majeshi ya ulinzi ya Iran kukiri kusababisha ajali ya ndege wiki iliyopita ambayo imeuwa watu wote katika ndege hiyo ya abiria.
Wakati huo huo Uingereza imemuita balozi wa Iran nchini humo leo kupinga kukamatwa kwa afisa wa ubalozi wa Uingereza mjini Tehran mwishoni mwa juma, serikali imesema.
London inataka kueleza kupinga kwake kwa nguvu kabisa juu ya ukiukaji mkubwa wa itifaki ya kidiplomasia, msemaji wa waziri mkuu Boris Johnson amesema leo. Msemaji wa serikali ya Iran Ali Rabiei akijibu swali kuhusu hatua hiyo ya Uingereza alisema:
„Hatua hii ya balozi wa Uingereza ni kinyume kabisa na kazi yake na haikubaliki na kwa kumuita katika wizara ya mambo ya kigeni tumewasilisha upinzani wetu kwa balozi na serikali ya Uingereza. Uingereza ina rekodi ya ripoti mbaya juu ya uingiliaji masuala ya ndani ya Iran."
Balozi Rob Macaire alikamatwa siku ya Jumamosi baada ya maandamno kuzuka katika kumbukumbu ya watu 176 waliofariki katika ajali ya ndege baada ya majeshi ya Iran kuidungua kwa makosa.