Armenia na Azerbaijan zaelekea kusuluhisha mvutano
16 Mei 2024Armenia na Azerbaijan zimefikia makubaliano juu ya sehemu zinazozozaniwa za mpaka wao wa pamoja, hatua mpya ya kurejesha uhusiano kati ya mahasimu hao wa kihistoria.
Makubaliano kati ya mataifa hayo mawili ya eneo la Caucasus, ambayo yote yalikuwa jamhuri za Kisovieti, yamefungua njia ya kurejeshwa kwa vijiji vinne vya mpakani vya Azabajan vilivyotekwa na Armenia katika miaka ya 1990.
Mwishoni mwa mwezi Machi, Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan alikubali kurudisha vijiji vinne vilivyotelekezwa ambavyo Yerevan iliviteka katika miaka ya 1990.Azerbaijan yakataa kushiriki mazungumzo ya amani na Armenia
Akizungumza wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri, leo Alhamisi, Pashinyan ametaja makubaliano hayo kama hatua muhimu ya kuimarisha zaidi mamlaka na uhuru wa Armenia.
Pashinyan alisema Armenia itajenga barabara mpya katika eneo hilo ndani ya muda wa miezi michache ijayo na walinzi wa mpaka wa nchi hizo mbili watawekwa kwenye mpaka uliochorwa upya "ndani ya siku 10 zijazo".
Armenia na Azerbaijan zilipigana vita mara mbili, katika miaka ya 1990 na mwaka wa 2020, kwa ajili ya udhibiti wa eneo la Nagorno-Karabakh.