Umoja wa Mataifa yaanza uchunguzi
12 Agosti 2015Vitendo hivyo vimefanywa na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwenye matukio tofauti. Kwa mujibu wa Shirika la Amnesty International, matukio hayo yametokea tarehe 2 na 3 ya mwezi huu wa Agosti katika eneo lenye Waislamu wengi kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui.
Shirika hilo limetoa madai hayo baada ya kuwahoji watu 15 walioshuhudia, huku wataalamu wa afya wakipata ushahidi wa unyayasaji wa ngono uliofanywa dhidi ya msichana huyo, baada ya kumfanyia uchunguzi.
Joanne Mariner, Mshauri Mwandamizi wa Mizozo wa Shirika la Amnesty International amesema uchunguzi wao unaonyesha kuwa mwanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, alimbaka msichana huyo mdogo na mwanajeshi mwingine aliwaua raia wawili. Amesema matukio hayo yametokea wakati ambapo wanajeshi wa kulinda amani kutoka Rwanda na Cameroon walikuwa wanaendesha operesheni kwenye mji wa Bangui.
Balla Hadji mwenye umri wa miaka 61 na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 16, Soulemaine Hadji, walipigwa risasi na kuuawa mbele ya nyumba yao. Aidha, msichana huyo alibakwa nyuma ya lori, baada ya mwanajeshi mmoja aliyekuwa amevalia kofia ya buluu ya jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa, kumtoa nje ya nyumba yao saa 8 usiku na kumpeleka nyuma ya lori hilo.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umeanzisha uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo za mauaji na ubakaji. Stephane Dujarric ambaye ni msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema tuhuma zote hizo zitachunguzwa kikamilifu.
Umoja wa Mataifa kutovumilia vitendo kama hivyo
''Tungependa kusisitiza kwa mara nyingine tena kuwa utovu wa nidhamu wa aina hii hauwezi kuvumiliwa na kwamba tuhuma zote zitachunguzwa vizuri na kwa umakini mkubwa,'' alisema Dujarric.
Dujarric amesema vitendo hivyo havikubaliki kabisa. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ameelezea kusikitishwa na kufadhaishwa na matukio hayo yaliyofanywa na wanajeshi wa kulinda amani wa umoja huo.
Madai hayo yanafuatia ukosoaji ambao umekuwa ukitolewa katika miezi ya hivi karibuni kutokana na taarifa za unyanyasaji wa ngono pamoja na ubakaji unaofanywa na wanajeshi wa kulinda amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kutozingatiwa kwa umakini.
Kwa mujibu wa taarifa za ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na mienendo na nidhamu, mwishoni mwa mwezi Juni, ziliripotiwa tuhuma za matukio sita ya unyanyasaji wa kingono na ubakaji uliofanywa na wanajeshi wa kulinda amani, tangu wanajeshi hao waingie nchini humo mwaka uliopita.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE,APE
Mhariri: Josephat Charo