1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa na Hali ya Jamhuri ya Afrika Kati

10 Aprili 2014

Wakaazi wa mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika kati Bangui wanasubiri kwa hamu matokeo ya kura ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuhusu mswaada wa azimio la kutumwa wanajeshi 12000 wa kulinda amani nchini humo.

https://p.dw.com/p/1Bf7p
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon na rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika Kati Catherine Samba-Panza(kushoto) wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na Afrika,Aprili 2, 2014 mjini BrusselsPicha: Reuters

Ufaransa inawasilisha mswaada wa azimio unaoshauri watumwe wanajeshi elfu kumi na askari polisi 1800 watakaoshika nafasi ya wanajeshi zaidi ya elfu tano wa kikosi cha nchi za Umoja wa Afrika kinachoungwa mkono na Umoja wa mataifa MISCA. Kikosi hiki kipya cha Umoja wa mataifa kitakuwa kikijulikana kama MINUSCA na hakitarajiwi kuanza shughuli zake kabla ya Septemba 15 mwaka huu.

Mswaada huo wa azimio unaelezea hofu kubwa zilizozuka kutokana na visa vinavyokwenda kinyume na haki za binaadamu na sheria za kiutu vinavyofanywa na makundi ya wanamgambo wa zamani tangu waasi wa Seleka mpaka wa Anti Balaka, ikiwa ni pamoja na mauwaji, kamata kamata ya ovyo ovyo, mateso, ubakaji wa wanawake na watoto na wengine kutojulikana waliko.

Mswaada huo wa azimio unayataka makundi yote ya wanamgambo na waasi yaweke chini silaha, yasitishe aina zote za matumizi ya nguvu, yaache kuvuruga utulivu wa nchi na yawatoe watoto wote wanaowatumia kama wanajeshi.

Jukumu la Kikosi cha MINUSCA litakuwa kuwahifadhi raia, kulinda misaada ya kiutu, kusimamia nidhamu na utawala wa mpito pamoja na kuhakikisha haki za binaadamu zinaheshimiwa.

Kundi la kwanza la wanajeshi wa Umoja wa ulaya limeshafika Bangui

Wakati huo huo askari wa Ufaransa - Gendarme - wanaotumikia kikosi cha nchi za Umoja wa Ulaya katika Jamhuri ya Afrika kati wameshaanza kupiga doria mjini Bangui katika wakati ambapo matumizi ya nguvu yanazidi kuenea nchini humo. Watu wasiopungua 30, wengi wao wakiwa raia wameuwawa jana kufuatia mapigano kati ya wanamgambo wa kikristo Anti Balaka na wale wa kiislamu. Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Ufaransa, kundi la kwanza la wanajeshi 55 wa Umoja wa Ulaya limewasili mjini Bangui. Wiki iliyopita Umoja wa Ulaya uliahidi kutuma wanajeshi 800 katika Jamhuri ya Afrika kati hadi mwishoni mwa mwezi ujao. Bunge la Ujerumani, Bundestag, linapiga kura kuhusu kushiriki wanajeshi wa Ujerumani katika juhudi za kulinda amani katika Jamhuri ya Afrika kati.

EU Afrika Gipfel Merkel 02.04.2014 Brüssel
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakikutana na wenzao wa Umoja wa Afrika,walizungumzia pia hali namna ilivyo katika jamhuri ya Afrika KatiPicha: Reuters

Nayo Marekani imetangaza msaada ziada wa kiutu wa dola milioni 22 kwa nchi hiyo inayosumbuliwa na kile katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon alichokiita "takasa takasa ya kikabila na kidini.

Mwandishi:Hamidou OummilkheirAP/AFP/dpa

Mhariri: Josephat Charo