1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Zoezi la uokoaji laendelea kutafuta waathiriwa wa India

Hawa Bihoga
4 Juni 2023

Waokoaji na wanafamilia leo Jumapili wameendelea kutafuta waathiriwa wa ajali mbaya ya treni nchini India, huku mawasiliano yakitajwa kuwa sehemu ya sababu ya kutokea kwa ajali hiyo.

https://p.dw.com/p/4SAgg
Indien Zugunglück in Balasore, Odisha
Picha: Dipa Chakraborty/Eyepix Group/IMAGO

Katika ajali hiyo iliotokea siku ya Ijumaa zaidi ya watu 288 wameuwawa wakati treni ya abiria ilipoacha reli na kugonga treni nyingine, karibu na wilaya ya Balasore katika jimbo la mashariki la Odisha.

Leo Jumapili miili mingine 5 imepelekwa katika shule ya jirani na ulipotokea mkasa huo ambayo inatumika kuhifadhi maiti.

Mamia ya watu wamejeruhiwa kwenye ajali hiyo inayotajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea ndani ya miongo kadhaa.

Soma pia:Idadi ya waliokufa kwa ajali ya treni India yafikia 280

Treni hizo ni Coromandel Express iliyokuwa ikisafiri kutoka Howrah, jimbo la Bengali magharibi kuelekea Chena, jimboni Tamil Nadu, na Howrah Superfast Express iliyokuwa ikisafiri kutoka Bengaluru huko Karnataka kuelekea Howrah.

Serikali yalaumiwa kwa "ukiritimba"

Shirika la reli India limesema, watu takriban milioni 13 hutumia huduma hiyokwa siku, lakini kutokana na kile ilichotaja "ukiritimba" wa serikali kumekuwa na rekodi mbaya ya usalama kutokana na miundombinu kutokarabatiwa.

Indien Zugunglück in Neu-Delhi
Kikosi cha waokoaji na raia wakiendelea kusaka waathiriwaPicha: DIBYANGSHU SARKAR/AFP

Ajali nyingi za treni zimekuwa zikitokea kila mwaka katika taifa hilo lenye mtandao mkubwa Zaidi wa reli duniani ulio chini ya usimamizi wa mamlaka moja.

Soma pia:Waokoaji hawajafanikiwa kupata manusura zaidi katika ajali ya India

Mwezi Agosti 1995, treni mbili ziligongana karibu na New Delhi na kusababisha vifo vya watu 358 katika moja kati ya ajali mbaya zaidi ya treni kuwahi kutokea India.

Mwaka 2016, treni ya abiria iliteleza na kuacha njia yake katikati ya miji ya Indore na Patna ambao watu 146 walifariki dunia. Makosa ya kibinadamu na vifaa vya kutolea ishara vilivyopitwa na wakati ndivyo vinavyolaumiwa kusababisha ajali nyingi kati ya hizo.

Waziri mkuu wa India Narendra Modi ambaye anakabiliwa na uchaguzi mwaka kesho, alitembelea eneo la mkasa hapo jana Jumamosi ambapo alizungumza na waokoaji pamoja na wahanga wa ajali hiyo.