Zimbabwe yatangaza hali ya maafa kutokana na ukame
5 Februari 2016Afrika Kusini pamoja na Zimbabwe,Malawi na Zambia zimeathiriwa vibaya na ukame uliopaliliwa na tukio la hali ya hewa linalojulikana kwa jina la El Nino na kusababisha kufa kwa maelfu ya n'gombe, mabwawa kupungukiwa maji na kushindwa kuvunwa kwa mazao yanayotegemea mvua.
Zimbabwe ambayo hapo zamani ilikuwa ikijulikana kama mzalishaji mkuu wa chakula barani Afrika imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa chakula wa mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni na imekuwa ikitegemea kuagizia nafaka kutoka nchi jirani kukidhi mahitaji yake.
Kutangazwa kwa hali ya maafa kunawezesha mashirika fadhili ya kimataifa kuharakisha upelekaji wa shehena za chakula wakati nchi hiyo yenye ukata wa fedha ikisema itanunuwa mahindi chakula kikuu nchini humo ili kuepusha njaa kwa umma.
Watu zaidi ya milioni 4 wakabiliwa na uhaba wa chakula
Waziri wa ujenzi wa Zimbabwe Savior Hasukuwere amesema katika taarifa awali kulikuwa na ishara kwamba watu milioni 1.5 wako hatarini kukabiliwa na ukosefu wa chakula ambapo kwa jumla vitongoji sitini vijijini vimeathirika.
Kwa jumla idadi ya watu hao ambao hawana usalama wa chakula imeongezeka na kufikia milioni 2.44 sawa na asilimia 26 ya wananchi wa nchi hiyo.
Mugabe amelaumu hali hiyo kutokana na mavuno kidogo kulikosababishwa na uhaba wa mvua kutokana na mabadiliko ya tabia nchi halikadhalika vikwazo vilivyowekwa na mataifa ya magharibi dhidi ya nchi hiyo kutokana na rekodi yake mbaya za haki za binaadamu.
Wakosoaji wa Zimbabwe wanasema uhaba wa chakula kwa kiasi fulani umesababishwa na sera ya rais ya mageuzi ya ardhi ya mwaka 2000 ambapo wakulima wa Kizungu waliondolewa kwa nguvu kwenye mashamba yao yenye rutuba ambayo yalitaifishwa na serikali.Baadae mashamba mengi yalikuwa hayatumiki kikamilifu.
Mifugo inakufa mazao yanyauka
Enos Jenhi mkulima katika kitongoji cha Masvingo mojawapo ya kitongoji kilichoathrika vibaya nchini Zimbabwe anasema mvua zimechelewa sana kunyesha kuweza kuyanusuru mahindi ambayo mengi yamenyauka na takriban n'gombe 16,500 wamekufa nchini humo.
Afrika Kusini imerokodi ukame mbaya kabisa tokea kuanza kuwekwa kwa rekodi zaidi ya karne moja iliopita.
Albert Fereira amekuwa akiendesha shughuli za kilimo katika shamba lake lilioko katika jimbo la Orange Free State kwa takriban miaka 60 sasa.
Anasema "Katu,katu katika maisha yangu sikuwahi kushuhudia ukame kama huu.Kwa kawaida katika kipindi hiki cha mwaka mahindi yanakuwa yamestawi na kupendeza. Lakini ardhi ilikuwa kavu sana tulishindwa kulima,hatukuweza kufanya chochote.Sasa hatuwezi kuotesha chochote ...tumechelewa mno..itabidi tusubiri msimu ujao."
Kwa kawaida Afrika Kusini husafirisha nje mahindi lakini sasa itabidi iagizie tani milioni tano mwaka huu ambazo ni nusu ya mahitaji yake.
Kwa mujibu wa Shirika la Taifa la masuala ya Bahari na Anga nchini Marekani mwaka jana kulikuwa na joto kali sana duniani kuwahi kushuhudiwa katika enzi ya sasa.
Mwandishi : Mohamed DahmanAFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga