1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe yashutumu Marekani kuhusu tangazo la uchaguzi

Mohamed Dahman26 Aprili 2008

Zimbabwe imeshutumu kuwa ni uongo mtupu tangazo lililotolewa na msaidizi waziri wa mambo ya nje wa Marekani Jendayi Frazer kwamba upinzani umepata ushindi wa wazi katika uchaguzi wenye utata wa mwezi uliopita.

https://p.dw.com/p/Dp1k
Jendayi Frazer msaidizi waziri wa mambo ya nje wa MarekaniPicha: AP Photos/Khalil Senosi

Waziri wa sheria Patrick Chinamasa amekaririwa akisema na gazeti la serikali la Herald kwamba Frazer hana mamlaka ya uadilifu au kisheria kutowa matangazo yasiokuwa na msingi kuhusu michakato ya ndani ya nchi nchini Zimbabwe na kwamba hata takwimu zilizochapishwa na chama cha MDC kwenye tovuti yake hapo tarehe pili mwezi wa April hazimfanyi Tsvangirai kuwa mshindi moja kwa moja.

Frazer amewaambia waandishi wa habari nchini Afrika Kusini hapo Alhamisi kwamba matokeo ya kuaminika kabisa waliyokuwa nayo ni ushindi wa dhahir wa Morgan Tsvangirai katika duru ya kwanza ya uchaguzi na yumkini hata ushindi kwa jumla.

Gazeti hilo la Herald pia limesema kwamba Tume ya Uchaguzi nchini Zimbabwe ZEC imetangaza matokeo zaidi ya majimbo mengine saba ya uchaguzi wa bunge wa mwezi uliopita.

Chama cha upinzani cha MDC kimeendelea kushikilia viti sita vya bunge wakati chama tawala cha Rais Robert Mugabe kimeshikilia viti vinne.Hakuna matokeo ya awali yaliobatilishwa.

Majimbo mengine kumi yaliobakia yanaoendelea kuhesabiwa upya yanashikiliwa na upinzani na chama cha Mugabe kinahitaji ushindi wa angalau viti tisa kuweza kulidhibiti tena bunge

Matokeo ya uchaguzi wa rais bado kutangazwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linazatamiwa kuarifiwa juu ya mzozo wa uchaguzi wa Zimbabwe hapo Jumanne.