1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe yafukuta

20 Januari 2011

Mgogoro unaongezeka kwenye serikali ya Zimbabwe kufuatia Mwanasheria Mkuu wa serikali, kuunda timu ya wanasheria watakaofanya uchunguzi juu ya iwapo waziri mkuu hawezi kufunguliwa mashtaka ya uhaini au ya kupanga njama.

https://p.dw.com/p/1002R
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe
Rais Robert Mugabe wa ZimbabwePicha: AP

Hii imetokana na kufichuliwa mwaka jana katika mtandao wa Wikileaks, ambao ulichapisha ripoti za siri za Wizara ya Mambo ya Marekani, juu ya Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai na uongozi wake wa chama cha MDC kuwa walikua na mipango na wanadiplomasia wa Kimarekani juu ya kuihamasisha Washington kutoa mchango wa kifedha ili kuwahonga maafisa wa usalama kubadilisha mfumo wa kiutawala nchini Zimbabwe.

Mwanasheria Mkuu Johannes Tomana aliwaambia waandishi habari kwamba timu ya wanasheria sita inayoangalia maswala ya Wikileaks imeshaanza kazi yake na itawasilisha mapendekezo yake mwisho wa mwezi Machi 2010.

Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai akizungumza na maafisa wa chama cha ZANU PF
Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai akizungumza na maafisa wa chama cha ZANU PFPicha: AP

Mwanasheria mkuu wa serikali alisema kuwa wanaoshiriki kwenye timu hiyo watabaki kuwa siri, ili kuleta kiwango cha juu cha ufuatiliaji kulingana na tuhuma hizo. Pia aliongeza kuwa hatojali kuhusu uwezekano wa kumchunguza Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai kama inaweza kuleta mpasuko kwenye serikali ya muungano ya Zimbabwe.

Kwa upande mwingine mwanasheria mkuu Tomana ni chanzo kimojawapo cha mgogoro kati ya Rais Robert Mugabe na Tsvangirai. Tsvangirai alimtuhumu Mugabe kwa kumteua Tomana kuwa mwanasheria mkuu wa serikali mtu ambaye alikua mtetezi wa chama cha Mugabe Zanu PF na uteuzi huo ulifanyika bila kumshirikisha.

Nelson Chamisa msemaji mkuu wa chama cha Tsvangirai cha Movement fo Democratic Change , MDC, alisema chama chake hakitakubali matokeo ya uchunguzi wa timu hiyo.

Mchambuzi wa maswala ya kisiasa MacDonald Lewanika alisema kuwa anaona kama kuundwa kwa kamati hiyo uchunguzi ni njia moja ya kuzusha matatizo na kuivunja serikali ya Umoja wa kitaifa, kuelekea uchaguzi ambao utafanyika baadae mwaka ujao .

Mwandishi: Mavhunga Columbus/ZR/Harrison Mwilima
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman