1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe tume ya uchaguzi yakubali ombi la ZANU-PF

Abdulrahman, Mohamed10 Aprili 2008

Waziri wa sheria amenukuliwa na redio ya Afrika kusini akisema kwamba ombi la ZANU-PF kutaka kura zihesabiwe upya katika majimbo matano

https://p.dw.com/p/DfRf
Rais Robert MugabePicha: AP


Waziri wa sheria wa Zimbabwe Patrick Chinamasa amenukuliwa na redio ya Afrika kusini akisema kwamba tumeya uchaguzi imelikubali ombi la ZANU-PF kutaka kura zihesabiwe upya katika majimbo matano. Chama hicho pia kimewasilisha malalamiko kupinga ushindi wa chama cha upinzani Movement for Democratic Change-MDC katika uchaguzi wa bunge la viti 210 tarehe 29 mwezi uliopita, kikidai kwamba MDC iliwahonga wapiga kura.


Kiongozi wa MDC Morgan Tsvangirai anaendelea kushikilia kwamba ameshinda uchaguzi wa rais kwa wingi wa kutosha na kuwa kushindwa kwa tume kutangaza matokeo hadi sasa kunathibitisha madai yake. Wadadisi wanasema inaelekea tume inashinikizwa na serikali.


Kinachosubiriwa na wazimbabwe kujua hatima ya uchaguzi huo, ni uamuzi wa mahakama kuu baada ya MDC kuwasilisha ombi la kuitaka mahakama iiamuru tume ya uchaguzi itangaze matokeo. Mahakama hiyo iliokutana jana mjini Harare, sasa itatoa hukumu yake Jumatatu ijayo.


Kwa upande mwengine , Bw Tsvangirai amesema chama chake kinaweka mlango wazi, tayari kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na baadhi ya wanasiasa wa ZANU-PF. Suala la kuundwa serikali ya aina hiyo tayari limeshapingwa na serikali ya rais Mugabe, ikisisitiza kwamba ni matokeo ya uchaguzi tu yatakayotoa muelekeo.


Hali nchini Zimbabwe inaonekana kuwatia dosari pia viongozi wa mataifa jirani na hasa katika jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC yenye wanachama 14 ambayo Zimbabwe ni mwanachama.Leo ikiwa ni siku ya 12 baada ya uchaguzi na matokeo ya kura za urais yakiwa bado hayajatangazwa, Mwenyekiti wa SADC , rais Levy Mwanawasa wa Zambia ameitisha kikao maalum cha wakuu wa nchi hizo jumamosi ijayo mjini Lusaka, kuzungumzia hali ya mambo na jinsi ya kuweza kuwasaidia Wazimbabwe. Mwanawasa amesema nia ni kujaribu kuondoa hali ya mkwamo iliojitokeza tangu uchaguzi.


Viongozi wa chama cha MDC wanasema wana matumaini kuwa wakuu wa Jumuiya ya SADC, watakua na ujasiri wa kumueleza bayana rais Mugabe mwenye umri wa miaka 84 kwamba sasa wakati umefika kuachia madaraka na kuinusuru Zimbabwe kutumbukia katika vurufu na machafuko, baada ya kuitawala kwa miaka 28 .


Hata hivyo wadadisi wana shaka shaka kama hilo litawezekana , kutokana na tabia ya muda mrefu ya baadhi ya viongozi hao kuoneana haya na kulindana , kama anavyosisitiza rai huyu wa Zimbabwe. anayeishi uhamishoni nchini Afrika kusini.


-O-Ton


Serikali ya Zimbabwe imesema inajiandaa kukiarifu kikao hicho cha jumamosi cha viongozi wa SADC mjini Lusaka , na naibu waziri wa habari Chris Matonge amethibitisha hivi punde kwamba rais Mugabe atahudhuria mkutano huo.