Zimbabwe na Palestina
24 Juni 2008Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wamechambua hali nchini Zimbabwe kabla ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais, mkutano wa Mashariki ya kati na juhudi za kukijenga upya kikosi cha polisi cha wapalestina na nusu-finali ya kesho ya kombe la Ulaya kati ya Ujerumani na Uturuki.
"Kila mara mtu anapoanza kuamini Zimbabwe haitatumbukia zaidi katika janga,rais Robert Mugabe na utawala wake wa kifisadi, unathibitisha kinyume chake:
Kuwadia tu duru ya pili ya uchaguzi,kampeni ya vitisho ya mtawala huyu wa kimabavu imefikia kilele chake.Matumaini yote ya kuwa na uchaguzi huru na bila ya m izengwe yametoweka zamani.
Kwa jicho la hali isio sawa ya kugombea duru hii ya pili ya uchaguzi,haisangazi kuona Upinzani umejitoa katika uchaguzi. Kwani, wiki kadhaa sasa Upinzani umekuwa ukiandamwa na Mugabe."
Ama gazeti la SCHWÄBISCHE ZEITUNG limegundua :
"Hata kiongozi mwenye nguvu mno kusini mwa Afrika -rais Thabo Mbeki, sasa anamkosoa ingawa si wazi wazi rais Mugabe.Wakati umewadia kwahivyo, kwa viongozi wa nchi za kiafrika, ladai gazeti-kuongeza shinikizo hatua kwa hatua kwa Mugabe.
Hii haitamfanya kuregeza kamba,lasema gazeti-lakini litawafanya wazimbabwe kupata moyo na kuonesha ushujaa mbele ya utawala ambao umeifilisi nchi.
Gazeti pia linawataka viongozi wa nchi za Ulaya kujaribu nyuma ya pazia kuwashinikiza viongozi wa Jumuiya ya SADC,lakini hadharani wafunge midomo yao .
Likitukamilishia maoni ya wahariri juu ya Zmababwe,gazeti la FRÄNKISCHER TAG linalochapishwa Bamberg linaona mkasa wa Zimbabwe ni ushahidi dhahiri-shahiri wa kushindwa viongozi wa Afrika kuisimamia nyumba yao isiporomoke.Laandika:
"Kwani hawaoni kuwa chama cha kidemokrasi cha upinzani nchini Zimbabwe kinapigana vita pekee bila ya msaada wao ? Matumaini ya upinzani kuungwamkono na jirani mkubwa Afrika Kusini yametoweka.Kinyume chake,gazeti ladai kimetokea:Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, anacheza karata zisizofahamika.Anajitokeza upande mmoja kama mpatanishi na kwa upande wapili anamtia shime Mugabe.
Likitugeuzia mada, gazeti la NEUE ZEITUNG linazungumzia mkutano wa Mashariki ya kati.Laandika:
"Kambi ya nchi za magharibi yafaa kuona ni kwa masilahi yake binafsi kuona Ukingo wa magharibi wa Mto Jordan una hali ya utulivu na imara.Kila wakaazi wake wakiishi maisha bora,ndipo hawata waungamkono wale wenye siasa na itikadili kali kama Hamas au kuangukia mikononi mwa Iran.
Ikiwa Ukingo wa magharibi utaangukia mikononi mwa chama cha Hamas kama mwambao wa Gaza-laonya gazeti-basi hakutakua na dola la wapalestina.
Endapo lakini, itafanikiwa kuunda taasisi kama polisi na Idara ya sheria huko ukingo wa magharibi,hapo msingi imara utakua umewekwa kuleta suluhisho la dola 2 na amani ya kudumu Mashariki ya kati.
WESTDEUTSCHE ZEITUNG kutoka Düsseldorf,lauchambua mpambano wa kesho wa nusu-finali ya kombe la Ulaya kati ya Ujerumani na Uturuki:Laandika:
"Kila kukicha, hamasa na jazba na hofu zinapanda nchini kuhusiana na changamoto hii.Huko Oberhausen, party kubwa mtaani imepigwa marufuku.Na hilo ni jibu la kawaida la wajerumani ambalo tunapaswa kuona aibu.Kwani, hakuna dalili yoyote ya kuzuka fujo..."