Zimbabwe na masoko ya bidhaa zake
19 Oktoba 2007Waziri Pheneas Chihota alitamka hayo alipohotubia bunge la Zimbabwe,mjini Harare.
Matamshi yake yameshangaza kwani, serikali ya Zimbabwe imeliweka mbele Bara Asia kama mshirika wake mkuu wa biashara na hasa China iliyoruhusiwa kuingia masoko ya Zimbabwe kwa urahisi.Zimbabwe ilikwenda umbali wa kuzindua sera maalum iliyolenga kutafuta masoko mapya kwa ajili ya mazao ya nyumbani.
Lakini mradi huo bado haujazaa matunda kama alivyoeleza balozi wa zamani wa Zimbabwe nchini China,Bwana Chris Mutsvangwa.Amesema,wafanya biashara wa Zimbabwe hawataki kushirikiana kibiashara na Wachina.
Hata matamshi ya waziri Chihota yametazamwa kama ni kukiri kuwa sera hiyo ya serikali,inayopuuzwa na Wazimbabwe imeshindwa kuleta maendeleo ya maana kunyanyua uchumi wa Zimbabwe unaozorota. Yadhihirika,serikali ya Zimbabwe imetambua kuwa Umoja wa Ulaya ni soko muhimu kwa mazao yake.
Waziri Chihota aliliambia bunge kuwa Umoja wa Ulaya pia ni mfadhili muhimu kabisa wa Zimbabwe. Akaunga mkono makubaliano ya ushirikiano wa biashara,kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za ACP yaani Afrika,Caribbean na Pacifik,yanayojadiliwa hivi sasa. Makubaliano hayo kwa ufupi EPA,yanapendekeza kuondosha ushuru wa forodha na vipimo vya sukari itakayouzwa na nchi za ACP.
Zimbabwe ni msafirishaji mkubwa wa sukari kutoka mashamba yake makubwa,yalio kusini-magharibi ya nchi.Kwa maoni ya Chihota,makubaliano ya EPA yakitiwa saini,Zimbabwe itaweza kuuza sukari yake kwa masharti yalio bora.
Wakati huo huo,Umoja wa Ulaya unasema,nchi kama vile Zimbabwe na Malawi zitanufaika sana na mapendekezo ya kuregeza masharti ya soko kuhusika na biashara ya sukari.Lakini hatua ya kuondosha ushuru wa forodha na viwango,inakwenda sambamba na uamuzi wa Umoja wa Ulaya kupunguza bei ya chini ya sukari,inayoweza kudhaminiwa.Kwani ifikapo mwaka 2009 bei hiyo itakuwa imeshuka kwa asilimia 36 na kuwa sawa na bei ya sukari duniani.
Kwa hivyo wazalishaji wa sukari nchini Malawi na Mauritius wakiwa na wasiwasi,wanataka kujua vipi hatua hiyo itaathiri uwekezaji mpya uliopangwa kufanywa katika viwanda vya sukari.
Kwa upande mwingine,takwimu rasmi zinaonyesha kuwa Zimbabwe katika mwaka 2006 iliagizia bidhaa za thamani ya Dola milioni 330 kutoka Uingereza na Ujerumani licha ya kuwepo mgogoro wa kisiasa kati ya Zimbabwe na nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani.
Serikali ya Zimbabwe,inatuhumiwa kukiuka haki za binadamu,ikiwa ni pamoja na kuwakamata na kuwatia ndani kiholela wale wanaotazamwa kama ni adui wa nchi.