1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe na kampeni ya kupiga vita polio

Jane Nyingi26 Juni 2007

Serikali ya Zimbabwe kwa ushirikiano na shirika la watoto la umoja wa mataifa –UNICEF imeanzisha kampeini ya mwezi mmoja inayonuia kuangamiza ugonjwa wa kupooza yaani polio na magonjwa mengine yanayowatatiza watoto. Kampeni hiyo ni ya kufuatilia nyingine kama hizo zilizofanywa katika miaka kadhaa iliyopita.

https://p.dw.com/p/CHkP
Picha: AP Photo
Kampeini hiyo ya kitaifa inanuia kutoa chanjo kwa watoto millioni mbili nchini Zimbabwe waliochini ya miaka mitano. Japokuwa taifa hilo lilitangaza mwaka wa 1999 kuwa halina matatizo ya ugonjwa wa kupooza liko katika hatari ya kupata maambukizi hayo kutoka nchi jirani kwa mfano Botswana. James Elder afisa mkuu wa mawasiliano wa unicef nchini zimbabwe akielezea juu ya kampeni hiyo alisema:

"Ni kampeini ya kitaifa lengo kuu likiwa kumfikia kila mtoto wa umri wa miaka mitano kwenda chini.Hadi sasa siwezi kusema idadi kamili ya watoto waliochanjwa lakini ni wazi kuwa imefanikiwa.tunataraji kufika kila sehemu ya Zimbabwe."

Kampeni hii inawadia wakati ambapo familia nyingi nchini Zimbabwe haziwezi kumudu gharama za afya kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, ukosefu wa ajira na idadi ya juu ya mayatima kutokana na ugonjwa wa ukimwi. Huduma za matibabu pia zimekuwa kero kwani hospitali nyingi nchini Zimbabwe pia zimelazimika kufungwa kutokana na ukosefu wa madawa na wahudumu wa afya kutorokea mataifa mengine ni kupata pato. Kampeni hiyo hasa inalenga maeneo ya mashambani ambapo huduma za matibabu ni nadra sana.

Katika maeneo hayo watoto waliochini ya miaka mitano watapata raundi ya kwanza ya chanjo ya ugonjwa huo wa kupooza kwa awamu mbili. Na watoto hawapewi tu chanjo ya ugonjwa wa kupooza bali hata magonjwa kama kifua kikuu, surua, dondakoo, pepopunda na homa ya majano - hepatatis B. Watoto hao waliochini ya miaka mitano pia walipata madawa ya kuongeza vitamin A mwilini. Foleni ndefu zilionekana katika mashule na makanisani ambayo sasa yamegeuzwa na kuwa mahala pa kupokea matibabu.

Shughuli hii inafanikiwa chini ya ufadhili wa uingereza,Ireland na Canada. Jumla ya dolla millioni moja zinatumika kugharamia utoaji chanjo, vifaa na malipo kwa matabibu. Foleni ndefu zilionekana katika mashule na makanisani ambayo sasa yamegeuzwa na kuwa mahala pa kupokea matibabu.Mbali na Zimbabwe kumeripotiwa ongezeko la ugonjwa wa kupooza katika matifa jirani kama vile Bostwana na Namibia. Shirika la unicef linatoa huduma zake katika zaidi ya mataifa 150 .