1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe kumuapisha Mnangagwa Ijumaa

23 Novemba 2017

Rais mtarajiwa wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, anajiandaa kuchukua rasmi madaraka baada ya Robert Mugabe aliyeitawala nchi hiyo kiimla kwa miaka 37 kujiuzulu

https://p.dw.com/p/2o7Nm
Simbabwe Emmerson Mnangagwa in Harare
Picha: Reuters/M. Hutchings

Rais mtarajiwa wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, anajiandaa kuchukua rasmi madaraka baada ya Robert Mugabe aliyeitawala nchi hiyo kiimla kwa miaka 37 kujiuzulu, huku ikifahamika kuwa kumefikiwa makubaliano yanayompa Mugabe kinga ya kutoshitakiwa.

Emmerson Mnangagwa ambaye ana uhusiano wa karibu na jeshi pamoja na wakuu wa usalama alirejea nchini Zimbabwe jana Jumatano kuchukua hatamu ya kuliongoza taifa hilo. Kwenye hotuba yake ya kwanza tangu alipofukuzwa kazi na Robert Mugabe mnamo Novemba 6 kwa kile kilichoonekana kuwa kushindania urithi wa kiti cha rais kati yake na mkewe Mugabe, Grace, Mnangagwa aliwaambia Wazimbabwe kuwa wanashuhudia enzi ya demokrasia kamili. Amesema lengo lake kuu ni kubuni nafasi za ajira na kuimarisha uchumi wa Zimbabwe ambao umezorota:

"Ninaahidi kuwa mtumishi wenu. Ninawasihi Wazimbabwe wazalendo kuungana pamoja, tushirikiane. Hakuna aliye muhimu kumzidi mwengine, sote ni Wazimbabwe. Tunataka kuujenga uchumi wetu. Tunataka amani nchini, tunataka kazi!Kazi! Kazi! Nchini mwetu."

Mitizamo tofauti kati ya ZANU-PF na upinzani

Emmerson Mnangagwa
Emmerson MnangagwaPicha: Reuters/M. Hutchings

Japo Mnangagwa alizungumzia kufanya kazi kwa ushirikiano, pia alinukuu baadhi ya kauli mbiu za chama cha ZANU-PF, jambo ambalo haliwapendezi wapinzani nchini humo, kwani ni kaulimbiu hizo ambazo hujenga hamasa ya kuwaona wapinzani kama si wazalendo kamili wa taifa lao na kuwanasibisha na wageni na mabeberu.

Waziri huyo wa zamani wa sheria na ulinzi amekuwa na uhusiano wa karibu na jeshi na alitekeleza vyema mikakati ya kiusalama ikiwemo ile ya kikatili katika serikali ya Mugabe, hali iliyompa jila la utani la Mamba.

Baadhi ya wafuasi wa upinzani wanaamini alihusika pakubwa wakati wa mauaji ya maelfu ya watu, pale Mugabe alipokabiliana na wapinzani wake mnamo miaka ya 80. Hata hivyo, Wazimbabwe wengi wanayo matumaini kuwa ataleta mabadiliko, kama Gift Bvunzawabaya, muuza maua katika mitaa ya mji mkuu, Harare: "Ninafikiri anaenda kufanya yale ambayo hayajafanywa na Mugabe. Tunamtaka rais huyo kutuunganisha na watu wengine na mabara mengine ili tuijenge nchi yetu."

Kinga kwa Mugabe?

Robert Mugabe na mkewe Grace
Robert Mugabe na mkewe GracePicha: Getty Images/O.Anderson

Wazimbabwe wanapojiandaa kumuapisha Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75 hapo kesho Ijumaa kuwa rais, swali ambalo watu wanajiuliza ni kuhusu hatima ya Robert Mugabe na mkewe.

Habari kutoka chanzo kilichokuwamo kwenye majadiliano ya kumtaka Mugabe aachie madaraka kimeliambia shirika la habari la Reuters hivi leo kwamba kulifikiwa makubaliano ya kumpa kinga kiongozi huyo ya kutoshitakiwa na pia kumuhakikishia usalama wake.

Mugabe mwenye umri wa miaka 93, alijiuzulu siku ya Jumanne na hivyo kumaliza utawala wake wa kiimla ambao umedumu kwa miaka 37. Hata hivyo hajaonekana hadharani tangu alipotoa hotuba yake iliyorushwa kwenye televisheni siku ya Jumapili.

Mwandishi: John Juma/AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef