1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe inaangamia-ulimwengu unakodoa macho

U.Schaeffer - (P.Martin)10 Desemba 2008

Kiongozi wa Zimbabwe Robert Mugabe anaiangamiza nchi yake;anazikiuka haki za binadamu.Na jumuiya ya kimataifa inatazama.Hilo ni jambo lisilowezekana.Je,utawala dhalimu wa Mugabe unakaribia mwisho wake?

https://p.dw.com/p/GD4Z
Women and children wait to collect water from an underground source following a water cut in Harare, Monday, Dec. 1, 2008. Water in the capital Harare was cut due to shortage of purification chemicals as Zimbabwe battles with a cholera outbreak which is thought to have left at least 425 people dead.(AP Photo/Tsvangirayi Mukwazhi)
Watoto na wanawake wakingojea kuteka maji Zimbabwe.Picha: AP

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Condoleezza Rice, Robert Mugabe anapaswa kungátuka.Wakati umewadia kwa jumuiya ya kimataifa kumshinikiza Mugabe kuondoka madarakani.Hayo pia ni maoni ya Ulaya.Kwa mujibu wa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Javier Solana,nchi zote 27 katika umoja huo zinakubaliana kuwa Mugabe lazima ajiuzulu.Alitamka hayo baada ya mazungumzo yake pamoja na mawaziri wa nje wa Umoja wa Ulaya mapema juma hili mjini Brussels.

Maneno hayo ni matamu masikioni hata ikiwa yamechukua muda kabla ya kutamkwa.Lakini yatawasaidia nini Wazimbabwe?Suala ni,nani atakaemngóa madarakani dikteta Mugabe anaengángánia kiti chake cha utawala?

Mtu hutamani kuwaambia wapitisha maamuzi mjini Brussels na Washington kuacha kutoa mito ya kisiasa iliyopangwa vizuri.Watu wa Zimbabwe hawana wakati wa kupoteza.Dikteta Mugabe anawaachilia raia wake kufa kwa njaa,nchi anaiangámiza,wapinzani wake na wenye uwezo wanatokomezwa.Je,mtu kweli anahitaji kukumbushwa kilichokuwemo katika Tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu linalosherehekewa leo hii kote duniani?

Wakati umewadia kutimiza kwa vitendo yale yanayotamkwa.Haitoshi kuimarisha tu vikwazo dhidi ya wawakilishi wa serikali ya Mugabe kama Umoja wa Ulaya unavyofanya au kupeleka tume za wataalamu kutenzua mzozo wa maji nchini Zimbabwe kama Afrika Kusini ilivyofanya.Haitoshi kupeleka misaada ya kiutu kwa mamilioni ya Wazimbabwe.Huu si mzozo wa huduma bali ni ukiukaji mkubwa kabisa wa haki za kimsingi za binadamu.Na jumuiya ya kimataifa ipo katika hatari ya kujipotezea uaminifu wake katika suala hilo hasa siku hii ya leo inayosherehekea Tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu.

Je,ingekuaje kama hayo yangetokea Ukraine au katika kanda ya Balkan?Je,jumuiya ya kimataifa ingejiamulia kuingilia kati?Bila shaka jawabu ni ndio.Yaonyesha kuwa mambo ni tofauti kabisa linapohusika bara la Afrika. Hapo,Ulaya na Marekani zingependelea kuona nchi za Kiafrika zikiwajibika zaidi.Kimsingi,hiyo ni sawa.Kwa hivyo wakati umewadia kuitisha mkutano wa viongozi wa Marekani,Ulaya na Umoja wa Afrika.Kwanini pande hizo tatu zinazotetea haki za binadamu zishindwe kukubaliana hatua ya kuchukuliwa kwa niaba ya umma wa Zimbabwe dhidi ya diketa alie madarakani?