Zimbabwe inaadhimisha miaka 28 ya Uhuru
18 Aprili 2008Kiongozi wa Zimbabwe,Roberrt Mugabe, anaekabilinana na shinikizo la kuondoka madarakani, anatarajiwa , leo Ijumaa, kutoa hotuba yake ya kwanza rasmi hadharani baada ya kufanyika uchaguzi wa utatanishi wakati wa kuadhimisha mika 28 ya uhuru wa nchi hiyo.Inatarajiwa katika hotuba hiyo kwa mara nyingine kuishambulia Uingereza.
Sherehe za miaka 28 ya Uhuru wa Zimbabwe za leo zimegubikwa na utata wa matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika wiki kadhaa zilizopita.
Hadi kufikia sasa,tume ya uchaguzi haijayatangaza.Sababu hazijulikani.Upande wa upinzani ambao unadai kuwa ulishinda uchaguzi huo unamlaumu Mugabe kwa sakata hii na kudai kuwa anapanga kubadili matokeo.
Mugabe alipangiwa kuhutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Gwazula ulioko katika kiunga cha jiji la Harare cha Highfield ambako wakati mmoja kilikuwa chimbuko la upinzani dhidi ya utawala wa weupe chini ya uongozi wa Ian Smith.
Hii ndio itakuwa mara ya kwanza kwa Bw Mugabe kuonekana hadharani tangu kufanyika kwa uchaguzi huo wa utata.
Mugabe, mwenye umri wa miaka 84,baado anachukuliwa kama shujaa katika nchi nyingi za kiafrika kutokana na mchango wake wakati wa kupigania ukombozi wa nchi hiyo katika miaka ya 70.Hata hivyo utawala wake unakabiliwa na tisho kubwa kuwahi kutokea tangu Uhuru wa nchi hiyo, uliotokea aprili 18 mwaka wa 1980.
Chama chake cha ZANU PF kilipoteza wingi wa viti bungeni katika uchaguzi wa Machi 29 na ingawa matangazo hayajatangazwa lakini upande wake tayari umekiri kuwa Mugabe ameshindwa kupata wingi wa kura dhidi ya mpinzani wake Morgen Tsvangirai katika uchaguzi wa urais.
Mugabe analaumiwa sana na mataifa ya magharibi kwa kile wanachosema kuwa ameharibu uchumi wa nchi hiyo kwa utawala wake uliodumu miaka 28.Kuna miito ya kumtaka anga'tuke na waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Condoleeza Rice aligusia jambo hilo kwa kusema kuwa ingawa ni suala la waZimabwe wenyewe ikiwa Mugabe anajiuzulu au la lakini kwa upande mwingine nchi hiyo imebadilika mdo miaka kumi na tano iliopita.na hali kwa sasa si ya kuridhisha.
Suala la Zimbabwe lilizungumziwa katika kikao maalum cha Umoja wa mataifa amabacho kiliitishwa na rais Mbeki kama aliepewa jukumu la kushughulikia suala la Zimbabwe.Lakini rais Mbeki alipinga kuzungumzia suala la masuala ya uchaguzi jambo ambalo lhalikumfurahisha kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgen Tsvangirai na kusema kuwa jukumu lake la upatanishi wa mgogoro wa kisiasa wa Zimbabwe na badala yake upewe mtu mwingine kama vile rais Levy Mwanawasa wa Zambia.
Kwa upande mwingine Tsvangirai amabe bila shaka hatahudhuria sherehe za leo amelaumiwa na serikali ya Mugabe kwa kuwa msaliti baada ya kudaiwa kuwa aliiomba serikali ya Uingereza kuingilia kijeshi katika nchi hiyo ambayo zamani lilikuwa koloni lake.
Madai hayo yamekanushwa na Tsvangirai pamoja na ubalozi wa Uingereza mjini Harare.
Hotuba ya Mugabe ya leo Ijumaa inaweza kuwa na mada ya kuipinga serikali ya Uingeraza kwani jana alhamisi alionekana akiwawambia vijana kuwa ni muhimu kulinda nchi hiyo dhidi ya ubepari wa Uingereza.