Zidane aanza kwa kishindo kama kocha wa Real
11 Januari 2016Mabingwa hao mara kumi wa Ulaya wanatumai kuwa “uwepo wa Zizou” inaweza kuirejesha klabu hiyo tajiri kabisa ulimwenguni katika mbinu za ushindi.
Kiungo huyo wa zamani wa Ufaransa na Real Madrid, aliyechukua nafasi ya Rafa Benitez aliwatazama vijana wake wakiwaangamiza Deportivo La Coruna tano sifuri katika mchuano wa La Liga ambao Garteh Bale alifunga matatu huku Benzema akiongeza mawili. Alimsifu Bale kutokana na mchezo wake "kazi ya Gareth lazima afanye ni sawa na wanayopaswa kufanya wengine. Kama hatuna mpira, wanapaswa kuwa pamoja, waulinde mlango, na wakati tukipata mpira, anapaswa kutafuta mianya na kucheza. Hicho ndio tunahitaji. Nna furaha na alichokifanya leo, sio rahisi kufunga mabao matatu katika mchuano mmoja.
Zidane alisema hakuwa na uwoga wowote kuhusu mchuano wake wa kwanza na kuwa bado vijana wake wanahitaji kuimarika "Leo ilikuwa changamoto nyingine. Ni muhimu kwangu kuwa hapa kama kocha na nataka kufutrahia hili. Nawashukuru mashabiki na nadhani kitu cha kwanza wao huja kuwaona wachezaji na leo wamefidiwa na ushindi wa timu. Kitu muhimu leo ni mtazamo wa timu. Tutaimarika, katika kila sehemu ya mchezo, tuna muda tuna wiki za kulifanyia hilo kazi na nna uhakika tutaimarika.
Real Madrid wanashikilia nafasi ya tatu pointi mbili nyuma ya Barcelona ambao wana mchuano wa ziada. Barca waliwazaba Granada nne bila mwishoni mwa wiki. Atletico Madrid wanashikilia usukani pointi mbili mbele ya Barca. Vijana hao wa kocha Diego Siemeone walipata ushindi wa mbili bila dhidi ya Cekta Vigo hapo jana.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohamed Khelef