Zidane aachia ngazi Real Madrid
31 Mei 2018Mwanasoka huyo wa zamani wa kimataifa aliye na umri wa miaka 45 ameamua kuondoka hivi sasa wakati angali katika nafasi ya juu akisema kwamba ilikuwa wakati wa mabadiliko kwake mwenyewe na klabu, na kukiri kwamba hakuwa na uhakika na uwezo wake wa kuendeleza rekodi ya ushindi akiwa Real.
Lakini amesema hakuna klabu nyingine iliyoshiriki katika uamuzi wake huo wa kuachana na Real ingawa wachambuzi wanasema Zidane anahusishwa na tetesi za kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa, ingawa mwenyewe amesisitiza kwamba kwa sasa macho yake yanatizama nafasi nyingine.
"Nimechukua uamuzi wa kutoendelea mwaka ujao kama kocha wa Real Madrid", alisema Zidane ambaye ni raia wa Ufaransa. "Klabu hii inastahili kuendelea kushinda na inahitaji mabadiliko", ameongeza Zidane na kusema anaamini muda ndio sasa.
Zidane ashuku uwezo wake
Zidane amesema hana uhakika kuhusu uwezo wake wa kuhamasisha timu kuendelea kupata ushindi zaidi. "Sijioni nikiendelea kushinda mwaka huu na mimi ni mshindi, sipendi kushindwa", ameongeza Zidane. "Nimefikiria sana juu ya uamuzi huu na siwezi kurudi nyuma".
Real iliichabanga Liverpool mabao 3-1 katika fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, Champions League mjini Kiev siku ya Jumamosi(26.05.2018), na kumfanya Zidane kuwa kocha wa kwanza katika historia kushinda mataji matatu ya Champions League mfululizo.
Zidane sasa ameshinda mataji 9 tangu alipochukua mikoba ya Rafael Benitez katika klabu hiyo ya Santiago Bernabeu mwezi Januari 2016.
Uamuzi wa kushutukiza
Rais wa klabu ya Real Madrid Florentino Perez amesema uamuzi wa Zidane "haukutarajiwa kabisa". Wakati Benitez alipotimuliwa Janurai 2016, gazeti la kila siku la mjini Barcelona la Mundo Deportivo liliandika kwamba Zidane alikuwa mtu wa kawaida ambaye angebadilishwa na kocha wa kudumu ndani ya muda mfupi.
Lakini Zidane alipata imani ya wachezaji na yaliyofuatia ni historia. "Hii ni siku ya huzuni", amesema rais wa klabu hiyo Perez.
Zidane amesema uamuzi wake huo hauhusiani na tetesi za nyota wa Real Cristiano Ronaldo za kwamba huenda akaondoka klabuni kufuatia ushindi wa Champions League siku ya Jumamosi.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi
Mhariri: Saumu Yusuf