Ziara ya waziri wa Uchumi Sigmar Gabriel China
2 Novemba 2016
Tunaanza na ziara ya siku tano ya waziri wa uchumi wa serikali kuu ya Ujerumani Sigmar Gabriel katika jamhuri ya umma wa China. Ziara hiyo inagubikwa na kishindo cha makampuni ya Ujerumani yanayolalamika dhidi ya vizuwizi wanavyokabiliana navyo nchini China. Gazeti la "Mitteldeutsche " la mjini Halle linaandika:"Wanasiasa wenyewe ndio wanaobeba jukumu la mashaka hayo. Kwa muda mrefu waliyafumbia macho mageuzi jumla na walishindwa pia kujiandaa kukabiliana nayo. Kwa muda mrefu serikali imekuwa ikiitetemekea China ingawa vizingiti vya kiuchumi kwa makampuni ya Ujerumani viko tangu miaka 30 sasa. Wakulaumiwa zaidi lakini ni wawakilishi wa sekta ya kiuchumi. Wamekuwa wakinyamaza ili kujiepushia madhara. Kwa pamoja lakini wameipoteza fursa, kwa ushirikiano pamoja na serikali kuu ya Ujerumani, kuishinikiza serikali ya mjini Peking, wakati ule ambapo Ujerumani ilikuwa na nguvu za kujadiliana. Hivi sasa lakini China imeshageuka kuwa dola kuu."
Kasheshe zagubika kampeni za uchaguzi wa rais Marekani
Kasheshe zinazidi kugubika kampeni za uchaguzi wa rais nchini Marekani. Na tangu shirika la ujasusi lilipotangaza kasheshe mpya ya barua pepe,upepo unaanza kuvuma upande mwengine. Gazeti la "Neue Osnabrücker" linaandika: "Mfululizo wa kasheshe hizo hasa ndio unaaomuathiri zaidi Hillary Clinton na kumfungulia njia mpinzani wake Trump kumpita katika utafiti wa maoni ya wapiga kura. Inazidi kudhihirika kwamba Clinton ni sehemu ya lile kundi la kichini chini la wenye usemi mjini Washington-sawa na taasisi yake. Wananchi wengi wamechoshwa na kundi hilo.Trump anazikosha nyoyo za wamarekani anaposema "atalisafisha bwawa la matope la Washington."Clinton anapigania kuendelea na hali ya mambo ,Trump anataka kuanzisha hali mpya. Pindi Clinton akishinda,na akila kitu kinaashiria hivyo,basi madowa hayo yataendelea kumsumbua. Hatoweza kamwe ,kuwasuluhisha wananchi baada ya kampeni hizo kali za uchaguzi."
Uturuki ina utawala wa kiimla
Hali nchini Uturuki na msimamo wa rais Tayyip Recep Erdogan inaendelea kugonga vichwa vya habari nchini Ujerumani. Gazeti la "Ludwigsburger Kreiszeitung" linaandika: "Uturuki ikiendelea hivyo hivyo,basi hapatopita muda,haitokuwa tena na mshirika. Ikiwa rais wa nchi hiyo anataka kurejesha adhabu ya kifo,Umoja wa Ulaya utabidi hapo hapo usitishe rasmi mazungumzo ya kuomba uanachama. Rais huyo anajidai walio wengi ndio waliomchagua. Lakini mfumo wa demokrasia unaovunja uhuru wa vyombo vya habari,unaotumia nguvu,unaovunja haki za jamii za wachache na haki za binaadam,si mfumo tena wa demokrasia,ni mfumo wa kiimla unaoungwa mkono na walio wengi. Na hivyo ndivyo watu wanavyobidi pia kuutaja.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga