Ziara ya Rais wa Ujerumani, Bwana Horst Koehler, nchini Ethiopia
14 Desemba 2004Bibi Kesten Müller alisema kwa kuisamehe Ethiopia deni la Euro milioni 67, Ujerumani inataka kuiunga mkono nchi hiyo katika mwenendo wa marekebisho yake ya kiuchumi. Alisema Wajerumani wanataraji kwamba fedha hizo zilizosamehewa zitatumiwa kupambana na umaskini nchini humo, kuendeleza mipango ya kutoa elimu zaidi au katika sekta za kilimo.
Kwa maneno hayo, Bibi Müller alitia mhuri wake, kwa niaba ya serekali ya Ujerumani, msamaha huo wa madeni.
Msingi wa mapatano hayo unatokana na mapatano yaliofikiwa na nchi fadhili ziliomo katika ile inayoitwa Klabu ya Paris ambayo ilitaka Ethiopia isamehewe asilimia 90 ya madeni yaliowekewa dhamana na serekali katika kuendeleza biashara ya kusafirisha nje bidhaa. Kansela Gerhard Schroader hapo mwezi Januari mwaka huu alipoitembelea Ethiopia alitangaza kwamba anataka msamaha huo uwe wa asilimia mia moja. Kwa ujumla, serekali ya Ujerumani tangu mwaka 1993 imeisamehe Ethiopia Euro milioni 197 zinazotokana na kuendeleza biashara. Ethiopia ni nchi inayotiliwa uzito sana na Ujerumani katika siasa yake ya ushirikiano katika maendeleo..
Bibi Kersten Müller alisema Ujerumani inataraji, kutokana na msamaha huo, hatua kwa hatua kutakuweko uongozi mzuri wa serekali, dimokrasia, kulindwa haki za binadamu katika nchi hizo. Alisema hakutaweza kuweko msamaha wa madeni bila ya masharti.
Mzozo wa mpaka baina ya Ethiopia na Eritrea umechipuka tena katika wiki zilizopita. Ethiopia haijaukubali mstari wa mpaka baina ya nchi hizo mbili uliochorwa na tume ya kimataifa ya upatanishi. Katika wiki iliopita, serekali ya Ethiopia , kwa upande wake, imetoa pendekezo jipya kuhusu masuala ambayo bado yanayobishaniwa.
Rais wa Ujerumani, Horst Köhler, amezungumza kwa urefu na waziri mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi, juu ya mzozo huo wa mpaka na akaelezea wasiwasi wake. Alisema amekwenda Ethiopia kuhakikisha kwamba Ujerumani inaunga mkono juhudi za kutafuta amani, kwa vile, jambo hilo, kwa uzoefu wake, kote katika Afrika, na hasa pia katika Ethiopia na Eritrea, pale panapokosekana amani katika nchi au eneo, basi hakutakuweko maendeleo mazuri ya kiuchumi na ya kijamii na kuukiuka umaskini. Kwa hivyo, amani lazima liwe lengo la juu kabisa katika eneo hilo ili kusaidia mapambano dhidi ya umaskini.
Kwa ujumla, Rais Köhler alipendezwa na maendeleo ya mwenendo wa dimokrasia katika Ethiopia. Katika ziara yake huko Addisababa, rais huyo wa Ujerumani alizinduwa jengo jipya la kituo cha utamaduni cha Ujerumani cha Goethe ambacho kitamalizwa kujengwa miezi michache ijayo. Rais huyo aliupongeza uhusiano baina ya nchi yake na Ethiopia ambao umekuweko kwa miaka mia moja sasa. Kesho Rais Koeler atamaliza ziara yake ya Ethiopia kwa kutoa hotuba katika jengo la Umoja wa Afrika, AU.
Miraji Othman