1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya rais Horst Köhler Korea ya kusini

Oumilkher Hamidou8 Februari 2010

Rais Köhler amesifu maendeleo ya kiuchumi na kitamaduni tangu mwaka 1986 hadi leo nchini Korea ya kusini

https://p.dw.com/p/Lvo8
Rais wa shirikisho Horst Köhler (kulia) na mkewe Eva Luise(kushoto) pamoja na rais Lee Myung-bak wa Korea ya kusini wanawaamkia watoto wakati wa sherehe mjini SeoulPicha: AP

Rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Horst Köhler amewasili Korea ya kusini baada ya ziara ya wiki moja nchini India.Mjini Seoul,rais Köhler amekutana na rais mwenzake Lee Myung Bak.Korea ya kusini ndio mwenyekiti wa kundi la mataifa 20 muhimu kiuchumi ulimwenguni-G20 kwa mwaka huu wa 2010.

Mgogoro wa fedha na kiuchumi ndio kiini cha mazungumzo atakayokua nayo rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Horst Köhler nchini Korea ya kusini."Nchi hizi mbili,Ujerumani na Korea ya kusini zinaweza kutoa mchango wa maana kumaliza mgogoro huo" amesema rais wa Shirikisho mwanzoni mwa ziara yake hiyo ya siku mbili.Leo asubuhi,rais Horst Köhler alikaribishwa kwa heshma za kijeshi na mwenyeji wake rais Lee Myung Bak,katika kasri la rais- Jumba la Buluu mjini Seoul.

Hii ni mara ya kwanza kwa rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Horst Köhler kufanya ziara rasmi mjini Seoul.Lakini anaijua vizuri Korea ya kusini tangu wakati alipokua mwenyekiti wa shirika la fedha la kimataifa IMF.Wakati wa mazungumzo yake pamoja na rais wa Korea ya kusini,rais wa shirikisho Horst Köhler alimkumbusha mwenyeji wake alifika kwa mara ya kwanza Korea ya kusini mnamo mwaka 1986.Wakati ule Seoul ilikua mwenyeji wa mkutano wa kila mwaka wa benki kuu ya dunia na shirika la fedha la kimataifa.

Mwaka huu pia Korea ya kusini itakaribisha mkutano wa kimataifa-viongozi wa kundi la mataifa 20 tajiri watakapokutana mjini Seoul,November 11 na 12 ijayo.

Kuhusu mkutano huo rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Horst Köhler amesema:

"Na mkutano wa mwaka utakaofanyika mwaka huu nchini Korea unamaanisha,ulimwengu mzima utatambua wakati huo kwamba Korea imefanikiwa kufanya maendeleo makubwa kiuchumi na kisiasa,na mie binafsi ,niruhusu mheshimiwa rais,niwapongeze wananchi wa Korea kwa ufanisi wa nchi yao kiuchumi na kitamaduni."

Ziara ya rais wa shirikisho imelengwa pia kushadidia uhusiano mzuri uliopo kati ya Ujerumani na Korea ya kusini.Rais Lee ameisifu Ujerumani kua ni mfano wa kuigizwa.Amesifu pia uhusiano wa jadi wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili pamoja na ushirikiano katika sekta ya kiuchumi,utamaduni na sekta nyenginezo.

Baada ya mazungumzo pamoja na rais Lee,rais wa shirikisho Horst Köhler amesema nchi zao mbili zinakubaliana panahitajika kanuni bayana kuweza kukabiliana na soko la fedha la kimataifa."Kila la kufanya linabidi lifanywe ili kuwaepushia walipa kodi balaa kama lile lililosababishwa na uzembe katika benki za uwekezaji."Amesisitiza rais Köhler.

Rais Horst Köhler amesifu juhudi za Korea ya kusini za kukabiliana na mgogoro wa fedha na kutia njiani sera madhubuti za kiuchumi.

Mwandishi:Marx,Bettina/ZR/ Hamidou Oummilkheir

Mhariri M.Abdul-Rahman