Ziara ya Papa nchini Uingereza
17 Septemba 2010Wakati kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita, akiendelea na ziara yake nchini Uingereza, polisi nchini humo wamewakamata watu watano kwa tuhuma za kuwa tishio dhidi ya kiongozi huyo. Watu hao wenye kati ya umri wa miaka 26 na 50 wamekamatwa, kulingana na sheria ya kupambana na ugaidi, katika duka moja mjini London.
Watu hao wanahojiwa katika kituo cha polisi cha London na bado hawajafunguliwa mashitaka yoyote. Polisi wamesema awali walilipekua duka hilo, lakini hawakugundua kitu chochote cha hatari. Polisi wamesema kuwa walipokea taarifa kuhusu vitisho dhidi ya Baba Mtakatifu, jambo lililosababisha operesheni ya wanajeshi kufanyika na hatimaye watu hao kukamatwa mapema leo asubuhi. Kutokana na tukio hilo, msemaji wa Vatican, Padri Federico Lombardi, amesema kuwa Baba Mtakatifu amefahamishwa kuhusu kukamatwa watu hao na amefurahishwa na taarifa kwamba hakuna mabadiliko yoyote yale ya ratiba katika ziara yake hiyo.
Kwa upande mwingine, Baba Mtakatifu amelikumbusha Kanisa Katoliki kuwa kipaumbele chake cha kwanza ni kuweka mazingira bora kwa watoto wadogo. Matamshi hayo ameyatoa mapema leo alipozungumza na walimu wa Kikatoliki. Hata hivyo, Baba Mtakatifu alikumbana na waandamanaji wanaoipinga ziara yake, pale mamia ya watu walipokuwa wakipiga makelele wakimtaka ajiuzulu wakati msafara wake ulipokuwa ukiingia katika shule moja ya Kikatoliki huko Twickenham, kusini-magharibi mwa London.
Akizungumza na waalimu na uongozi katika Kikanisa dogo la shule hiyo, kiongozi huyo ya Kanisa Katoliki duniani alisema kuwa shule za Kikatoliki hazina budi kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya watoto na vijana. Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Uingereza wameshughulikia kwa haraka visa vya kunyanyaswa watoto kingono vilivyofanywa na mapadri wa Kanisa hilo, kuliko ilivyokuwa kwa Ireland au Marekani. Baba Mtakatifu alisema ataendelea kuomba hilo liendelee kwa ajili ya kurudisha imani na ubora katika shule za Kikatoliki.
Mapadri waliohusikana na vitendo hivyo walikuwa wakihamishwa kutoka parokia moja kwenda nyingine, badala ya kuvuliwa madaraka na kukabidhiwa kwa polisi. Suala hilo limetoa changamoto kubwa sana katika uongozi wa miaka mitano wa Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita, ingawa visa vingine vilifanyika miongo kadhaa iliyopita. Baadae leo Baba Mtakatifu atakutana na kiongozi wa Kanisa la Kianglikana duniani, Askofu Mkuu wa Cantebury, Rowan Williams huko London, ambapo pia atahudhuri Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na askofu huyo katika Kanisa Kuu la Westminster Abbey.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (APE/RTRE)
Mhariri:Miraji Othman