Ziara ya Erdogan na biashara ya silaha magazetini
19 Mei 2014Tuanzie lakini na biashara ya silaha ya Ujerumani inayotishia kugeuka mwiba wa mchongoma katika njia ya waziri wa uchumi Sigmar Gabriel.Gazeti la Braunschweiger Zeitung linaandika:"Ikiwa mkondo wa mageuzi unamuwia mgumu,basi kwanini waziri anaweka matumaini makubwa?Mtu aliyesema "ni fedheha" kwamba Ujerumani ni miongoni mwa mataifa yanaosafirisha silaha kwa wingi duniani,na baadae kuruhusu silaha hizo hizo zipelekwe katika nchi za kiimla,hajipandishii hadhi yake.Ikiwa Sigmar Gabriel hatogutuka,basi sera ya biashara ya silaha inaweza kumgeukia na upande wa upinzani tayari unavizia."
Gazeti la Frankfurter Rundschau linaangalia uwezekano wa kutekelezwa mageuzi na kuandika:"Ujerumani inasafirisha silaha nyingi zaidi kuliko China,Japan,Ufaransa na Uingereza.Zaidi ya hayo makampuni ya silaha yanatuma manuari za kimambo leo ,vifaru au vifaa vya kutengenezea silaha hadi katika nchi zinazokumbwa na mizozo.Waziri wa uchumi Sigmar Gabriel anasema anataka kuiwekea vizuwizi sera ya biashara ya silaha.Lakini suala linalozuka ni vipi? Hata sheria kuhusu biashara hiyo,mfano uchunguzi kuhusu biashara ya silaha zinazotumika vitani au sheria kuhusu biashara ya nje hazijafafanuliwa kikamilifu.Serikali kuu ya Ujerumani italazimika ifafanue na iimarishe sheria hizo ikiwa inataka kweli kutekeleza sera ya amani na usalama na sio kutumikia masilahi ya makampuni yanayotengeneza silaha."
Erdogan awavunjia matumaini waturuki ya kujiunga na Umoja wa Ulaya
Ziara iliyopangwa kufanywa na waziri mkuu wa Uturuki,Recep tayyeb Erdogan mjini Cologne ambako amepangiwa kuhutubia katika uwanja wa michezo wa Lanxess Arena May 24 inazusha mabishano.Waziri mkuu wa Uturuki anatuhumiwa kutaka kuitumia ziara hiyo kufanya kampeni ya uchaguzi,ili achaguliwe kama rais nchini mwake.Kuna wanaomtaka Erdogan aifutilie mbali ziara hiyo.Gazeti al "Saarbrücker Zeitung" linaandika:"Akija Cologne na kuhutubia kama inavyodhaniwa basi atakuwa anaitumia vibaya Erdogan haki kama mgeni na wakati huo huo kuichafua hadhi ya waturuki nchini Ujerumani.Anawatumia kwaajili ya kuendeleza sera zake za malumbano.Na anavuruga,siku moja kabla ya uchaguzi wa bunge la ulaya,matumaini ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya kwasababu, kila mtu atatambua kuanzia Ujerumani hadi kufikia kwengineko barani Ulaya ,Uturuki ikiendelea kuwa na waziri mkuu kama huyu haitaweza kamwe kuwa mwanachama wa umoja wa Ulaya.
Kampeni chapwa za uchaguzi wa bunge la ulaya
Ripoti yetu ya mwisho inahusu uchaguzi wa bunge la Ulaya utakaoitishwa jumapili ijayo.Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika:"Kampeni sabaa za uchaguzi kwaajili ya bunge jipya ndizo zilizofanywa hadi wakati huu.Na hakuna hata moja iliyoacha kumbukumbu.Pengine katika kampeni ya nane mambo yatakuwa tofauti.Kwa mara ya kwanza kuna wagombea watano wakuu wanaopigania pia wadhifa wa mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya kupitia kura ya wananchi.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman