1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky: Nchi za kiarabu zisifumbie macho uvamizi wa Urusi

19 Mei 2023

Rais wa ukraine Volodymyr Zelensky amewashutumu baadhi ya viongozi wa mataifa ya Kiarabu kwa kupuuza matukio mabaya yanayosababishwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4RahP
Saudi-Arabien | Ankunft Wolodymyr Selenskyj in Dschidda
Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine akiwasili mjini Jeddah, Saudi Arabia kuhudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Picha: Saudi Press Agency/REUTERS

Akizungumza katika mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Jeddah, Zelensky amesema kuna baadhi ya viongozi hao wanaopuuza hatua ya Urusi ya kunyakuwa baadhi ya maeneo yake. Zelensky amewataka viongozi wa jumuiya hiyo kuviangalia vita hivyo kwa jicho la haki na ukweli.

Ziara ya kushtukiza ya Zelensky katika Mashariki ya Kati ni ya kwanza tangu Urusi ilipoivamia Ukraine zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Hata hivyo, maafisa wa jumuiya hiyo wamesema mualiko wa rais huyo wa Ukraine umetoka kwa kiongozi wa Saudi Arabia na sio jumuiya nzima.

Mkutano huo pia umemkaribisha tena Rais wa Syria Bashar al Assad katika vikao vyake baada ya kumpiga marufuku kwa miaka 12 tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipozuka nchini mwake mwaka 2011.