1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky awasilisha "Mpango wa Amani" kwenye Umoja wa Ulaya

17 Oktoba 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewasilisha "Mpango wa Ushindi" kwenye Baraza la Umoja wa Ulaya, wakati akisaka uungwaji mkono zaidi inapojiandaa na Mkutano wa Amani unaotarajiwa kufanyika siku zijazo.

https://p.dw.com/p/4lv2E
Volodymyr Zelensky
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amewasilisha Mpango wa Amani kwa Baraza la Ulaya na kuomba kuungwa zaidi mkono na muungano huo pamoja na wa kijeshi wa NATOPicha: The Yomiuri Shimbun/AP/picture alliance

Rais Volodymy Zelensky wa Ukraine amelihutubia Baraza la Umoja wa Ulaya mjini Brussels na kuwasilisha ''Mpango wa Ushindi' wa taifa hilo huku akiwasisitizia washirika wake kwamba Ukraine inahitaji uungwaji mkono thabiti kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na hasa katika wakati inapojiandaa kwa ajili ya mkutano ujao wa amani. 

Rais Volodymyr Zelensky aliwasili Brussels na kukaribishwa na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel. Jambo kubwa lililompeleka Brussels ni kuwasilisha mpango wa ushindi wa Ukraine mbele ya viongozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya pamoja na mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Zelensky alisisitiza haja ya upatikanaji wa haraka wa dola bilioni 35, zinazotokana na mali ya Urusi ili kuimarisha uwezo wa ulinzi wa Ukraine na kusisitiza udharura huo wa kuungwa mkono inapojiandaa na juhudi zijazo za kidiplomasia.

''Mpango wa Ushindi' ni daraja la Mkutano wa Pili wa Amani wenye mafanikio. Mnaweza kusaidia kulifanya hili kuwa dhahiri. Na hii itailinda sio tu Ukraine, bali pia mataifa ya kanda ya Baltiki, Nordic, Poland na Balkan, na maeneo mengine, na washirika wengine ambao wanalengwa na Urusi.''

Brüssels EU-Mkutano wa kilele | Zelenskyj, Charles Michel na Orban
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamesisitiza kwamba wataendelea kuiunga mkono Ukraine katika vita dhidi ya Urusi, katika Mkutano wa Kilele mjini Brussels, Oktoba 17, 2024Picha: NICOLAS TUCAT/AFP

Amesema Urusi itatumia diplomasia pale tu itakapoona kwamba haiwezi kupata chochote kwa kutumia nguvu na kuongeza kuwa mpango huu ndio hasa kinachohitajika na kuna umuhimu wa kutengeneza mazingira sahihi ili kumaliza vita baina yao na Urusi.

Kiongozi huyo wa Ukraine tayari ameizuru miji mikuu ya Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uingereza, kutangaza mpango wake huo.

Victor Orban aukosoa mpango wa Zelensky

Michel pamoja na Rais wa Bunge la Ulaya Roberta Metsola wamesisitizia juu ya uungwaji mkono usioyumba wa umoja huo kwa Ukraine, na kutoa wito wa kuisaidia haraka kijeshi na kifedha, na kusisitiza kwamba mustakabali wa Ukraine upo mikononi mwa Umoja wa Ulaya na kwamba wanauona mpango huo kama njia ya kusonga mbele.

Ubelgiji Brüssels | Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya
Viongozi wa Umoja wa Ulaya pamoja na Rais Volodymyr Zelensky wakiwa kwenye picha ya pamoja katika mkutano wa kilele wa Umoja huo mjini Berlin, Oktoba 17, 2024Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Waziri Mkuu wa Hungary na mshirika wa karibu wa Urusi, Viktor Orban hata hivyo, ameukosoa mpango huo wa Zelensky na kuzitaka Ufaransa na Ujerumani kwa niaba ya Umoja mzima wa Ulaya, kuanza mazungumzo na Urusi haraka iwezekanavyo. Orban, ni rais wa sasa wa umoja huo.

Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte hii leo amemuhakikishia Zelensky kwamba anao uungwaji mkono kutoka mataifa 32 wanachama na watafanya chochote kinachotakiwa kuhakikisha Ukraine inashinda.

Pendekezo la Zelensky pamoja na mengineyo linapinga makubaliano yoyote ya kimaeneo na wito kwa washirika wa Magharibi kuondoa vikwazo vya kutumia silaha za masafa marefu za Magharibi kuyalenga maeneo ya kijeshi ya Urusi.

Katika hatua nyingine, Rais Zelensky amesema nchi yake imepata taarifa za kijasusi kwamba Korea Kaskazini inajiandaa kupeleka wanajeshi 10,000 kuungana na vikosi vya Urusi kupigana na Ukraine na kuonya kwamba, hatua kama hiyo ya taifa la tatu kujiunga kwenye mzozo huo, inaweza kuugeuza na  kuwa "vita vya dunia."