1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky asaini mkataba wa 'kihistoria' na Ujerumani

16 Februari 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametia saini mkataba wa usalama na Ujerumani , uliopongezwa na Kansela Olaf Scholz kama "hatua ya kihistoria" inayoimarisha uungaji mkono endelevu.

https://p.dw.com/p/4cUkj
Deutschland | Münchener Sicherheitskonferenz | Wolodymyr Selenskyj
Picha: Thomas Kienzle/AFP/Getty Images

Katika mstari wa mapambano Ukraine imesema inajiondoa katika viunga vya kusini mwa mji wa Avdiivka. 

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amepata msaada mpya wa kijeshi na kutia saini mkataba wa muda mrefu wa usalama na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Berlin katika mkutano wa usalama uliogubikwa na habari za kifo cha mkosoaji wa serikali ya Urusi Alexei Navalny.

Mkataba huo wa usalama, ambao utadumu kwa miaka 10, unajumuisha pia ahadi ya Ujerumani kuendelea kuisaidia Ukraine kijeshi na kuiwekea Urusi vikwazo na udhibiti wa biashara ya nje. Berlin pia imetayarisha kifurushi kingine cha msaada wa haraka chenye thamani ya euro bilioni 1.13 ambazo zinalenga kuimarisha ulinzi wa anga na silaha.

Soma pia: Zelensky azitembelea Berlin, Paris kusaka msaada zaidi

Akizungumza katika mkutano wa huo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz  amesema  "Leo tunaweka pamoja kifurushi kingine cha msaada wa kijeshi chenye thamani ya euro bilioni 1.1 kwa Ukraine. Miongoni mwa mambo mengine, ni pamoja na vifaru 36 na mizinga ya kurusha makombora, risasi 120,000 za mizinga, mifumo miwili ya ziada ya ulinzi wa anga ya Skynex, na makombora yanayohitajika haraka aina ya Iris-T.  Lakini leo pia tunapiga hatua ya kihistoria, mimi na Rais Zelensky tumetia saini ahadi za muda mrefu za usalama baina ya nchi.

Zelensky ameishukuru serikali ya Ujerumani na watu wa Ujerumani kwa kuiunga mkono nchi yake kwa kifurushi kipya cha msaada wa kijeshi. Aidha rais huyo atasaini makubaliano kama hayo na Ufaransa wakati akitafuta msaada kwa vikosi vyake, ambavyo vinatatizika kudhibiti mashambulizi ya Urusi kwenye mji ulio mstari wa mbele wa Avdiivka.

Ofisi ya rais wa Ufaransa ilithibitisha kuwa makubaliano ya usalama yatatiwa saini Ijumaa jioni, lakini haikutoa maelezo yoyote kuhusu maudhui yake.

Shinikizo linazidi Avdiivka

Ukraine | Russische Soldaten bei Awdijiwka
Askari wa kikosi cha Ukraine akipiga doria.Picha: Genya Savilov/AFP/Getty Images

Katika uwanja wa mapambano kamanda wa jeshi la Ukraine amesema wanajeshi wake wanaopiga doria katika mji wa Avdiivka mashariki mwa Ukraine wako chini ya shinikizo kubwa.

Soma pia: Hali ngumu kwa wanajeshi wa Ukraine walioko mashariki

Uchambuzi uliofanywa na taasisi ya Marekani inayofuatilia vita (ISW) imesema wanajeshi wa Urusi walikuwa wamesonga mbele kutoka maeneo kadhaa, huku picha zikionyesha jeshi la Urusi likisonga mbele kutoka kaskazini na kupanda kuelekea katika mji wa Avdiivka. 

Huku haya yakijiri Ukraine imesema kuwa inajiondoa katika nafasi yake kwenye mstari wa mbele wa vita kwenye viunga vya kusini mwa mji wa Avdiivka, ambapo mapigano makali yalikuwa yakiendelea na vikosi vya Urusi.

Kupitia mtandao wa kijamii, Jenerali wa Ukraine upande wa mashariki, Oleksandr Tarnavsky, amesema "baada ya miezi mingi ya makabiliano, vikosi vyake vimeamua kujiondoa kwenye nafasi ya Zenit kwenye viunga vya kusini mashariki mwa Avdiivka, akisema wamefikia uamuzi huo ili kuokoa wafanyikazi na kuboresha hali ya utendaji.