Zelensky apendekeza makubaliano ya fidia kutoka Urusi
21 Mei 2022Zelenskiy, ambaye anasema Urusi inajaribu kuharibu miundombinu ya Ukraine kwa kadri inavyoweza, ameongeza kuwa mpango kama huo utaonyesha mataifa yanayopanga vitendo vya uchokozi kwamba yatalazimika kulipia matendo yao. Katika hotuba yake kupitia njia ya video, Zelenskiy amesema kuwa wanakaribisha mataifa yote washirika kutia saini makubaliano ya kimataifa na kuunda utaratibu wa kuhakikisha kwamba kila mtu aliyeathirika kutokana na vitendo vya Urusi anaweza kupokea fidia kwa hasara aliyopata.
Zelenskiy amesema chini ya makubaliano kama hayo, pesa na mali ya Urusi katika mataifa yaliotia saini makubaliano hayo zitazuiwa na kuelekezwa katika hazina maalumu ya fidia. Mwezi uliopita, Canada ilisema kuwa itabadilisha sheria zake za vikwazo kuwezesha mali ya nje iliyozuiwa kutumiwa kama fidia kwa waathiriwa ama kusaidia taifa la nje kujijenga upya baada ya vita.
Urusi yadai kuchukuwa udhibiti Mariupol
Huku hayo yakijiri, Urusi Ijumaa imedai kuchukuwa udhibiti wa mji wa bandari wa Mariupol nchini Ukraine katika kile kitakachokuwa ushindi mkubwa zaidi katika vita vyake na Ukraine baada ya takriban miezi mitatu ya mapigano yaliosababisha uharibifu mkubwa katika mji huo na vifo vya takriban raia elfu 20. Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu aliripoti kwa rais Vladimir Putin ''ukombozi kamili'' wa kiwanda cha chuma cha Azovstal huko Mariupol hii ikiwa ngome ya mwisho ya Ukraine. Haya ni kwa mujibu wa msemaji wizara ya ulinzi ya Ukraine Igor Konashenkov.
Hakukuwa na uthibitisho wa haraka kutoka Ukraine.
Shirika la habari la serikali ya Urusi RIA Novosti limeinukuu wizara hiyo ya ulinzi ikisema takriban wapiganaji 2,439 wa Ukraine waliokuwa wamejificha katika kiwanda hicho cha chuma walijisalimisha tangu Jumatatu ikiwa ni pamoja na wengine zaidi ya 500 waliojisalimisha Ijumaa. Wakati wa kujisalimisha, wanajeshi hao walichukuliwa kama wafungwa na vikosi vya Urusi na baadhi yao wanasemekana kulazwa hospitalini.