Zelenskiy: Lazima kurejea kwenye mazungumzo na Urusi
5 Aprili 2022Wakati hayo yakiendelea Rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev amesema ripoti za mauaji ya raia huko Bucha zilikuwa za uongo na zililenga kuidhalilisha Urusi.
Rais Zelenskiy amesema hayo alipokuwa akielekeza shutuma zake kwa vikosi vya kijeshi vya Urusi kwa kutekeleza mauaji ya Raia kiholela katika mji wa Bucha uliopo magharibi mwa mji mkuu wa Ukraine Kyiv.
Amesema matukio yaliotokea katika mji wa Bucha hayawezi kusamehewa lakini Ukraine na Urusi zinapaswa kuchukua chaguo gumu la kuendeleza mazungumzo.
Soma zaidi:Ukraine yailaumu Urusi kwa uhalifu wa kivita
Akigeukia misingi ya kisheria, amesisitiza lazima wanajeshi wa Urusi wafikishwe mbele ya sheria kwa vitendo vya kikatili kwa raia wasio na hatia.
Akizungumza katika ujumbe wa video Zelenskyy ameishutumu wazi Urusi kwa kujaribu kupotosha ukweli na kuanzisha kile alichokiita kampeni ya uongo iliobeba dhima ya kuficha hatia yao ya mauaji ya raia katika mapambano yanayoendelea katika maeneo muhimu nchini Ukraine.
" Tayari wameanzisha kampeni ya kudanganya ili kuficha hatia yao ya mauaji ya raia huko Mariupol. watawauwa watu makusudiili ionekane kama wameuwawa." Alisema Zelenskiy katika ujumbe wake wa video uliosambazwa.
Ameongeza kuwa pengine wavamizi hao wanajaribu kuficha athari za uhalifu wao. "Hawakufanikiwa kufika Bucha walipokuwa wakiondoka, lakini huenda ikawezekanakatika maeneo mengine."
Aidha ameongeza kwamba hali ya kijeshi katika mji wa bandari ya kusini wa Mariupol imekuwa ikikabiliana na mazingira magumu katika juhudu za kuwarudisha nyuma wanajeshi wa Urusi.
Rais wa zamani Urusi Medvedev aingilia kati shutuma hizo
Wakati Ukraine ikiishutumu wazi vikosi vya urusi kutekeleza mauaji ya raia, Rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev alisema ripoti za mauaji ya raia huko Bucha ni za "Uongo" na zinalenga kuidhalilisha Urusi.
"Propaganda wanazoziendeleza ni za uongo, na fikra wanazozijenga ni za kijinga." Dmitry Medvedev, ambaye aliwahi kuwa rais kutoka 2008 hadi 2012 na sasa ni naibu katibu wa Urusi Baraza la Usalama, alisema.
Soma zaidi:Zelensky azuru mji wa Bucha nje ya jiji la Kyiv
Moscow imesema itawasilisha ushahidi wa kitaalamu katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne kuthibitisha kuwa aihusiki katika mauaji hayo.
Hali mjini Bucha itachukuliwa kama ushahidi dhidi ya uhalifu wa kivita
Mataifa ya Magharibi yamesema kuwa raia waliokufa ni ushahidi wa uhalifu wa kivita. Shirika la habari la Reuters liliona maiti katika mji wa Bucha lakini halikuweza kuthibitisha nani alihusika na mauaji hayo.
Nchi za Magharibi zimeapa kuiwekea Urusi vikwazo zaidi baada ya kupatikana kwa raia wengi waliokufa, wengine walipigwa risasi vichwani.
Rais wa Marekani Joe Biden siku ya Jumatatu alimshutumu Rais wa Urusi Vladimir Putin wa uhalifu wa kivita na kuonesha nia ya kufungua kesi.
"Mliona kilichotokea Bucha, hii inamuakisi yeye ni mhalifu wa kivita" Biden aliwaambia waandishi wa habari mjini Washington.
Soma zaidi:Ukraine yachukua udhibiti wa eneo la Kyiv kutoka kwa Warusi
Tangu wanajeshi wa Urusi walipoondoka katika miji na vijiji vilivyozunguka mji mkuu wa Kyiv wanajeshi wa Ukraine wamekuwa wakionyesha maiti za watu wanaodaiwa kuwa ni raia waliouwawa na vikosi vya Urusi,nyumba zilizoharibiwa na magari yaliyoteketezwa.
Katikati ya hali hiyo Uturuki imependekeza mpango wa kuwahamisha raia waliojeruhiwa na maiti kutoka katika jiji hilo, lakini imeonya kwamba mpango huo utategemea na mapenzi ya rais wa Urusi Vladimir Putin.
Chanzo:Mashirika