ZEC yamtangaza Shein mshindi kwa 91%
21 Machi 2016Uchaguzi huo uliogomewa na upinzani ulifanyika kwenye mazingira ya utulivu sana, lakini ukishuhudia kiwango kidogo cha wapigakura. Waandishi wa DW kwenye maeneo mbalimbali ya visiwa vya Unguja na Pemba waliripoti vituo vya kupigia kura vikiwa na watu wachache, huku maafisa usalama na wa ZEC wakionekana kungojea kwa muda kabla ya wapigakura kuingia.
Akitangaza matokeo hayo kwenye ukumbi wa Salama katika Hoteli ya Bwawani mjini Unguja, Jecha alisema Dk. Shein alipata asilimia 91.4, na hivyo kufanya vyama vingine vilivyoshiriki kwa hiari au vilivyojikuta vinalazimishwa kushiriki kukosa hata asimilia 10, ambazo kisheria zingeliweza kukifanya chama chengine kualikwa kwenye serikali ya umoja wa kitaifa.
Jecha aliufuta uchaguzi wa awali wa tarehe 25 Oktoba 2015 kwa madai ya kuwepo kasoro kubwa, hatua ambayo ilipingwa vikali na Chama cha Wananchi (CUF), ambacho aliyekuwa mgombea wake wa urais, Maalim Seif Sharif Hamad, anasema alikuwa ameshinda kwa zaidi ya 52%.
CUF haiutambui uchaguzi
Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa CUF upande wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, aliiambia DW kwa njia ya simu kwamba chama chake kiligomea uchaguzi wa marudio kwa kuwa haukuwa halali. Hata hivyo, aliwashukuru wananchi kwa kuonesha kiwango kikubwa cha uwelewa, utulivu na kudumisha amani "hata baada ya kuchokozwa, kupigwa, kuteswa na kudhalilishwa" na vyombo vya dola.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai, alisema chama chake kimeridhishwa na namna ZEC ilivyouendesha uchaguzi wa marudio kinyume na ule wa Oktoba 25, ambao chama hicho na Jecha wanadai uliharibika.
Dk. Shein, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2010 alipotangazwa mshindi kwa tafauti ndogo ya kura mbele ya Sharif, anatazamiwa kuapishwa Jumanne, katika sherehe ambazo zitafanyika kwenye Uwanja wa Amaan, kando kidogo ya kitovu cha mji wa Zanzibar.
CUF ilisema awali kuwa isingeliyatambua matokeo yanayotokana na uchaguzi huo, na hivyo changamoto kubwa kabisa ya muhula huu wa utawala wa Dk. Shein inatarajiwa kuwa ni kupambana na upinzani mkali wa kisiasa kutoka chama hicho chenye nguvu kubwa.
Bado haijafahamika ikiwa Dk. Shein ataunda serikali nyengine yenye muundo wa umoja wa kitaifa, kwani - mbali na chama chake, CCM - hakuna chama chengine kilichotangaziwa na ZEC kufikia asilimia 10 ya kura za jumla wala kupata wajumbe kwenye baraza la wawakilishi, masharti muhimu kwa chama kualikwa kwenye uundaji wa serikali kwa mujibu wa katiba ya visiwa hivyo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf