1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zanzibar yazindua teknolojia yakutambua maambukizi ya corona

16 Februari 2022

Zanzibar imezindua teknolojia itakayowezesha kutambua maambukizi ya Covid-19, kwa muda wa saa mbili baada ya kupimwa kwa kutumia vipimo vya skana ama smaku umeme.

https://p.dw.com/p/477MM
Sansibar | President Dr Hussein Mwinyi
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amesema kuwa teknlojia hiyo itawapa afueni maelfu ya watalii wanaozuru kisiwa hicho. Uzinduzi wa teknolojia hii mpya kabisa barani Afrika unajiri huku virusi vya corona vikiendelea kubadilika badilika, huku baadhi ya mataifa yakiwa na hofu ya kuwepo kwa vipimo bandia.

Teknolojia hii inaondoa nafasi ya vipimo feki. Rais wa  Zanzibar Dokta Hussein Mwinyi amesema kuwa teknolojia hiyo itawaondolewa usumbufu wasafiri. Kwa kawaida kwa msafiri wa ndege anaihitaji kupimwa saa 24 kabla ya kuabiri ndege ila sasa teknlojia hii itamwezesha kupimwa na kupata matokea kwa kipindi kifupi katika uwanja wa ndege.

"Tumefanya makubaliano na Sunmade, ambayo ni kampuni ya Abu-dhabi, kuleta mashine maalum inayoitwa EDE scan, ambayo watu watakuwa wanapita tu na kutambuliwa kama wana covid.” alisema rais Mwinyi

Ugonjwa Covid-19 ulipobisha hodi Zanzibar, uliacha makovu katika uchumi wake unaotegemea utalii. Utalii huchangia asilimia 30 ya jumla ya pato la taifa. Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2020 Zanzibar ilikuwa inapokea watalii 500,000, lakini virusi vya corona vikapunguza idadi hiyo hadi 117,000.

Teknolojia yaleta afueni Zanzibar

Tansania Sansibar | Coronavirus | Impfung Ahmed Nassor Mazrui, Gesundheitsminister
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui akipokea chanjo ya COVID 19 hivi karibuniPicha: Salma Said/DW

Teknojia hii ni afueni kwa Zanzibar kwani ndege za Umoja wa Falme za Kiarabu zilizokuwa zimepigwa marufuku sasa zitaanza kuingia huku ndege ya Shirika la Abu Dhabi likianza usafiri wake leo kwa kuleta mitambo minne.

“Hata mtu akiwa na dharura akisafiri anaweza akapata majibu chini ya dakika 30 au lisani moja.” Alisema DadKarim Mulla  Mkurugenzi wa kampuni ya Alfacare Group ambayo imeufadhili mpango huu.

Kwenye mpango huo, watalii ambao watakuwa wanaingia Zanzibar na hawajachanjwa watakuwa wakipokea chanjo ya COVID-19, bila malipo kwa kwa njia salama na rahisi bila taabu ya kustahimili kifaa kilichozoeleka katika kupima virusi vya corona kwa njia ya pua maarufu kama usufi wa pua.

Mazungumzo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Tanzania bara yanaendelea kuhusu uwezekano wa teknolojia hii kutumika bara. Mataifa mengine ya Jumuiya ya Afrika Mashariki hayajaanza kutumia teknolojia hii mpya. Kuhusu viwango vya maambukizi ya virusi vya corona hapa Zanzibar, Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui amesema kuwa ni vidogo ila Wazanzibari wanahitaji kuchukua tahadhari.

Skana hizi ni za kwanza na za kipekee barani Afrika na zinaiweka Zanzibar kuwa nchi ya kwanza kihistoria kutumia teknolojia hii, katika mapambano dhidi ya Jangaa la COVID-19. Teknolojia hii ambayo pia inatumika katika Umoja wa Falme za Kiarabu itahakikisha kwamba wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wanapata huduma muafaka na bora ulimwenguni.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, DW, Zanzibar