Zanzibar. Kazi ya kuhesabu kura inaendelea.
31 Oktoba 2005Kazi ya kuhesabu kura inaendelea leo Jumatatu baada ya uchaguzi wa rais na bunge katika kisiwa maarufu cha utalii cha Zanzibar ambako kama katika chaguzi zilizopita kumekuwa na ghasia na madai ya kughushi.
Mgombea wa chama cha upinzani Seif Sharif Hamad amedai kuwa anaongoza dhidi ya rais wa sasa Amani Karume ilipofika usiku wa Jumapili, licha ya kuwa hakuna matokeo rasmi ya mwanzo yaliyotolewa.
Kiasi cha watu saba wamejeruhiwa, wawili kwa risasi na wengine watano kwa mapanga ama kwa fimbo, kwa mujibu wa daktari mmoja katika hospitali ya mjini humo.
Daktari huyo ambaye hakutana kutajwa jina lake amesema risasi hizo zimefyatuliwa na polisi.
Nje ya kituo kimoja cha uchaguzi katika eneo la mji mkongwe, majeshi ya usalama yalifyatua risasi pamoja na mabomu ya kutoa machozi , kuwatawanya waungaji mkono wa chama cha CUF waliokuwa wakipinga dhidi ya kuwepo kwa wapiga kura walioletwa na chama tawala cha CCM.
Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo.