1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Zanzibar itakuwa kama Dubai"

Salma Said22 Oktoba 2015

Wakati kampeni za uchaguzi mkuu nchini Tanzania zinaelekea ukingoni, ahadi nzito zimechukuwa nafasi kubwa katika kampeni za mwaka huu. Wananchi wanaamini kuwa ahadi hizo zinaweza kutekelezwa?

https://p.dw.com/p/1Gsc9
Mabango ya kampeni Zanzibar
Picha: DW/M. Khelef

Licha ya vyama 14 kusimamisha wagombea urais hapa Zanzibar, ushindani mkubwa unaonekana upo katika vyama viwili vya CCM na CUF ambavyo wagombea wake wa urais muda wote wa kampeni wamekuwa wakitoa ahadi bila kujali uzito wa kutekelezaji wa ahadi hizo, kila mgombea ameahidi kuwafanyia mengi wananchi iwapo atamchaguliwa.

Ahadi hizo ni kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ambayo imetolewa na mgombea wa chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad huku mgombea wa Chama Cha Mapinduzi CCM Dk Ali Mohammed Shein akiahidi kuigeuza Zanzibar kuwa Dubai.

Swali la kujiuliza ni jee ahadi hizo zinatekelezeka kwa kiasi gani? Hawa hapa baadhi ya wananchi wanazungumzia utekelezaji wa ahadi hizo.

Maalim Seif Sharif Hamad ameahidi kuifanya Zanzibar kama Singapore
Maalim Seif Sharif Hamad ameahidi kuifanya Zanzibar iwe kama SingaporePicha: DW/M. Khelef

Wananchi wana imani na viongozi

"Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatekelezeka kwa asilimia 100," anasema Hamis Hamis. "Kwa mfano, ahadi za elimu. Dokta Shein amesema watajenga skuli za ghorofa. Juzi amesema atajenga chuo cha mali na vyuo vya mali vimeshajengwa Mkokotoni na kwengineko. Kwahiyo nahisi hivi vitu vinatekelezeka."

Naye Juma Hamis Juma anaamini kuwa ahadi za Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF pia zinatekelezeka. "Aliwahi kuwa kiongozi pamoja na mzee Ali Hassan Mwinyi na tuliona mambo yalibadilika katika hii nchi kwa hiyo tuna imani kubwa kuwa ana uwezo wa kufanya kitu hicho, angalau kwa asilimia 85."

Ahadi nyengine ambao zimekuwa zikitolewa na vyama vyote, hata vile ambavyo havina wafuasi wengi, ni kuimarisha huduma za kijamii, kurekebisha mfumo wa elimu, miundombinu na kutoa huduma za afya bila ya malipo, kuongeza ajira kwa vijana, kufufua viwanda vilivyokufa pamoja na kuongeza mishahara kwa wafanyakazi. Suala la kurejesha mamlaka kamili ya Zanzibar, na kupitia mfumo wa Muungano, kuyatoa mafuta na gesi asilia kwenye Muungano na kuikwamua katiba mpya ambayo imekwama, limechukua nafasi katika kampeni za wagombea mwaka huu.

Vijana wa Zanzibar wanaongojea uchaguzi mkuu
Vijana wa Zanzibar wanaongojea uchaguzi mkuuPicha: DW/M. Khelef


Jumla ya vyama 14 vimesimamisha mgombea wa urais wa Zanzibar lakini ushindani mkubwa upo kwa vyama vya CCM na CUF ambavyo wananchi wengi ndio wenye kwenda katika mikutano na kusikiliza sera za vyama hivyo ingawa na hivyo wingine vinapata watu wachache.

Mwandishi: Salma Said

Mhariri: Hamidou Oummilkheir