ZANU PF wataka kura zihesabiwe upya
6 Aprili 2008Harare:
Chama tawala cha ZANU-PF nchini Zimbabwe kimetoa mwito kura za uchaguzi wa rais uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita zihesabiwe tena.Gazeti linalomilikiwa na serikali la Sunday Mail limesema chama tawala kimewasilisha maombi hayo mbele ya kamisheni ya uchaguzi kufuatia madai ya makosa yaliyotokea katika zowezi la kuhesabu kura.Tangazo hilo limetolewa muda mfupi baada ya mgombea wa upande wa upinzani wa Vugu vugu la mageuzi ya kidemokrasi MDC,Morgen Tsvangirai kumtuhumu rais Robert Mugabe kutaka kubadilisha matokeo ya uchaguzi ambayo mpaka sasa bado hayajatangazwa.Chama cha MDC kinasema Morgen Tsvangirai ameshinda kataika uchaguzi wa rais wa March 29 iliyopita.Wakati huo huo MDC kinapanga kutuma malalamiko mengine mahakamani ili kuilazimisha kamisheni ya uchaguzi itangaze matokeo ya uchaguzi wa rais.Jana polisi waliwazuwia wafuasi wa MDC wasiingie katika jengo la korti kuu mjini Harare.Kamisheni ya uchaguzi imetangaza matokeo ya uchaguzi wa baraza la Senet,ambapo vyama vyote viwili,ZANU PF na MDC vimejikingia idadi sawa ya viti.Kila upande umenyakua viti 30 kati ya 60 vya baraza hilo la Senet.Itafaa kusema hapa kwamba chama cha upimzani cha MDC kimeshinda katika uchaguzi wa bunge.