Zaidi ya watu milioni 1 duniani wafa kwa COVID-19
29 Septemba 2020Kulingana na takwimu za Chuo Kikuu cha Johns Hopkins zilizotolewa Jumanne, idadi hiyo ya maambukizi ya maradhi ya COVID-19 yameripotiwa kwenye zaidi ya nchi 210 tangu kisa cha kwanza kilipogunduliwa nchini China, kwenye mji wa Wuhan Desemba, 2019.
Shirika la Afya Duniani, WHO linatabiri kuwa idadi ya vifo inaweza ikaongezeka mara mbili, iwapo hatua za kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona hazitazingatiwa ipasavyo. Marekani inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya vifo ambapo hadi sasa imerekodi vifo 205,047, ikifuatiwa na Brazil, India, Mexico na Uingereza.
Merkel na wasiwasi kuhusu maambukizi
Nchini Ujerumani, Kansela Angela Merkel anatafuta njia ya kukubaliana kuhusu hatua madhubiti za kupambana na COVID-19 kama vile kuzuia mikusanyiko na vizuizi katika maeneo yanakouza pombe, wakati akijiandaa leo kukutana na viongozi wa majimbo 16 wa Ujerumani.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika mkutano wa chama cha CDU, Merkel alisema Ujerumani inaweza ikarekodi maambukizi mapya 19,200 kwa siku iwapo watu wataendelea kuzipuuza hatua zilizowekwa za kuzuia virusi vya corona visisambae. Jana taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukizwa ya Ujerumani, Robert Koch ilirekodi visa vipya 1,192 na vifo vipya vitatu na kuifanya idadi jumla ya maambukizi kufikia 285,332 na vifo 9,460.
Msemaji wa Kansela Merkel, Steffen Seibert amesema kiongozi huyo ana wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa maambukizi na amewasihi wananchi kuchukua hatua za afya ambazo zimewekwa ikiwemo kuvaa barakoa, iwapo wameshindwa kutekeleza agizo la kukaa umbali wa mita 1.5 kati yao. ''Hatuwezi kuruhusu virusi hivi visambae tena kwa kasi kwenye maeneo binafsi. Kwa masikitiko tunaona ni wapi jambo hili linawapeleka baadhi ya marafiki zetu wa Ulaya,'' Seibert
Nchi nyingine duniani
Aidha, Ufaransa, Uholanzi na nchi kadhaa za Ulaya zimeimarisha vizuizi wakati ambapo maambukizi ya COVID-19 yakiongezeka. Kwa upande wake Urusi imerekodi visa vipya 8,135, huku wanasiasa nchini humo wakipuuza uvumi kwamba shughuli za nchi nzima zitafungwa kwa awamu ya pili.
Watu nchini Uingereza wanaweza wakakabiliwa na faini ya hadi Pauni 1,000 kwa kutojiweka katika karantini baada ya kuambukizwa virusi vya corona. Kwa mujibu wa masharti mapya yaliyoanza Jumatatu, faini hiyo inaweza kuongezeka hadi Pauni 10,000 kwa watu watakaorudia kosa hilo.
Huko Israel, Waziri wa Afya, Yuli Edelstein amesema ''hakuna njia'' kwamba nchi hiyo itaondoa hivi karibuni sheria zilizowekwa za kuzifunga tena shughuli za nchi nzima kwa mara ya pili kwa muda wa wiki tatu.
Nako barani Afrika, shirika la WHO limetangaza mpango wa kuzisaidia nchi zenye uchumi mdogo na uchumi wa kati kuongeza vifaa vya upimaji wa COVID-19. WHO na washirika wake kadhaa wanapanga kutoa vifaa milioni 120 vya kupima virusi vya corona kwa baadhi ya nchi, zikiwemo nchi 20 za Afrika.
(DPA, AP, AFP, Reuters, DW https://bit.ly/33bMPnu)