Zaidi ya watu 40,000 waachwa bila makaazi Afrika Mashariki
2 Julai 2020Shirika la Wakimbizi la Norway limesema kuwa zaidi ya watu 40,000 kwenye eneo la Afrika Mashariki walilazimishwa kuondoka kwenye makaazi yao tangu mwezi Machi na kuwaweka katika hatari ya kuambukizwa virusi vya Corona. Shirika hilo limeomba kusitishwa kwa muda hatua ya kuwaondoa watu hao wakati wa janga hili.
Wanaoathirika zaidi ni watu waliokimbia machafuko, ukame na mafuriko kutoka Somalia, huku wengine wanaoishi katika maeneo yasio rasmi nchini Kenya na Ethiopia wakijikuta bila mahali pa kuishi baada ya makaazi yao kuvunjwa.
Mshauri wa kisheria wa shirika hilo la wakimbizi la Norway kwenye eneo la Afrika Mashariki, Evelyn Aero, amesema kuondolewa makwao kwa watu hao kunawaweka katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya corona kutokana na msongamano na maeneo yasiyo safi wanakoishi sasa.
Aero amesema watu waliofukuzwa makwao hawana usalama wa kifedha na wengi wao tayari wamepoteza ajira zao kutokana na janga la virusi vya corona na wamejikuta bila mahali pa kuishi. Amesema wengine wana njaa na wako katika kitisho cha kupatwa na ugonjwa wakati ambapo tunatakiwa kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kuwakinga watu wote.
Wengi miongoni mwa wathirika ni masikini
Shirika la habari la Reuters limesema kuwa juhudi za kuwapata maafisa wa serikali za Kenya, Somalia na Ethiopia kwa ajili ya kuelezea hali hiyo hazikufua dafu. Maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 hayana kasi zaidi barani Afrika ukilinganisha na Asia na Ulaya, lakini nchi zote 54 tayari zimeripoti maambukizi.
Kwa mujibu wa taasisi za kudhibiti magonjwa barani Afrika, bara hilo lina visa laki nne vilivyoripotiwa, vikiwemo vifo 10,000. Afrika Mashariki imerikodi visa 36, 000. Aidha wataalamu wa kiafya wanaelezea kwamba idadi ya visa vya virusi vya corona inaweza kuwa kubwa kuliko ilivyoripotiwa kutokana na kwamba baadhi ya nchi hizo zina mapungufu ya vifaa vya kupima wagonjwa.
Shirika la wakimbizi la kimataifa la Norway NRC linasema kwamba ni nchi ya Somalia iliyokumbwa na machafuko ya miongo mitatu, ambako kuna idadi kubwa ya watu waliofukuzwa makwao.
Toka kuripotiwa kwa janga la COVID-19 mwezi Machi, zaidi ya watu 34,700 walifukuzwa na wamiliki wa ardhi kwenye makaazi yao kwenye miji ya Mogadishu, Baidoa na Hargeisa. Nchini Kenya takribani watu 7,000 zikiwemo familia za mzazi mmoja na watoto walivunjiwa maakazi yao na serikali kwenye maeneo ya Kiriobangi na Ruai.
Kwenye nchi jirani ya Ethiopia watu wapatao 1,000 walijikuta pia bila makaazi mwezi Aprili, baada ya viongozi wa mji wa Addis Ababa kuvunja makumi ya maakazi yao ambayo walisema walinunua kinyume na sheria.
Wanaharakati nchini Kenya wanasema kwamba wengi miongoni mwa waathirika ni masikini, wanaotegemea pato ya kila siku na ambao walipoteza ajira kutokana na janga la virusi vya corona.