Zaidi ya watu 150 waangamia katika ajali ya ndege Uhispania
21 Agosti 2008Miongoni mwa watu 182 waliokuwa ndani ya ndege hiyo ya Shirika la ndege la Spainair, watu 19 tu ndio wamenusurika.
Ajali imetokea wakati ndege hiyo ilikuwa katika hatua ya mwanzo ya kuruka kutoka uwanja wa ndege wa Barajas mjini Madrid na kushika moto. Msemaji wa kundi moja la waokozi anatoa ushahidi wake: ´´Kulitokea ajali wakati ndege ikijaribu kupaa kutoka sehemu ya nne ya uwanja wa ndege. Muda mfupi baada ya kutoka, ndege iliripuka kutokana na sababu isiojulikana´´.
Viongozi wa huduma za ndege huko Uhispania wanasema ndege hiyo aina ya Boeing ya kampuni ya ndege ya Uhispania ya Spainair, ilikuwa ikielekea katika visiwa vya mapumziko vya Canary.
Hadi sasa haijajulikana ni sababu gani imepelekea ajali hiyo lakini viongozi wameanza uchunguzi. Asili ya abiria waliouawa haijulikani pia lakini inasemekana kulikuwa na raia kutoka nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Uhispania, Ujerumani, Sweeden na Uholanzi.
Risala za rambi rambi kutoka kwa viongozi wa mataifa mbali mbali duniani zimefikishwa kwa waziri mkuu wa Uhispania Jose Luis Zapatero na mfalme Juan Carlos. Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev, amesema amehuzunishwa na taarifa kwamba kumetokea ajali ya ndege kwenye uwanja wa ndege wa mjini Madrid na kusababisha vifo vya watu wengi kiasi hicho. Rais wa Italy, Giorgio Napolitano, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, ni miongoni mwa viongozi wa nchi wameshatuma risala zao za rambi rambi.
Wataalamu wa kisayikolojia wapato 170 wanajaribu kuwahudumia ndugu, jamaa na marafiki wa wahanga wa ajali hiyo mjini Madrid na mjini Las Palmas visiwani Canary.
Msiba wa siku tatu umetangazwa katika mji wa Madrid na eneo lake.
Ajali hiyo ndio ajali mbaya kuwahi kutokea nchini Uhispania tangu ajali ya tarehe 19 Februari mwaka 1985 kaskazini mwa nchi ambapo watu 148 waliuawa. Na ajali mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani ni yile iliyotokea visiwani Canary tarehe 27 mwezi Machi mwaka 1977 ambapo ndege mbili aina ya Boeing ziligongana na kusababisha mauaji ya watu 583.