Zaidi ya watu 130 wauawa na moto Australia
9 Februari 2009
Moto huo uliyotokea mwishoni mwa wiki umeteketekeza vitongoji kadhaa vinavyozungukwa na misitu katika jimbo la Victoria kusini kaskazini mwa Australia.
CLIP: SHEPHERD 1
´´watu ambao walidhani ya kwamba wamesalimika, chini ya sekunde chache tu nyumba zao zilizingirwa na moto na hakukuwa na nafasi hata ya kutoka nje kwa mlango wa mbele au nyuma au kukimbilia kwenye magari yao´´
Ni msemaji wa polisi katika Jimbo la Victoria Phil Shepherd akielezea namna watu walivyokumbwa na maafa hayo.
Moto huo ambao chanzo chake inaarifiwa kuwa ni hali ya joto kali pamoja na upepo, umeteketeza zaidi ya nyumba 750 ambapo miji katika jimbo hilo yote imeteketea.Mji wa Kinglake sasa umebaki jina tu katika ramani.
Zaidi ya hekta laki tatu za msitu nazo pia zimeketekezwa na moto huo unaoendelea kuwaka, huku maelfu ya wafanyakazi wa kupambana na moto pamoja na waokoaji wakiendelea na juhudi za kuuzima na kuwakoa wahanga.
Waziri Mkuu wa Australia Keniv Rudd ameelezea tukio hilo kama ni maafa ya halaiki, na kutangaza msaada wa kiasi cha dola millioni 6.8 na kwamba juhudi zaidi za kuwasaidia wahanga zinafanyika.
CLIP:RUDD
´´Tunalazimika kufanya kile kinachotakiwa kufanywa kuisaidia kila jamii ili irejee katika maisha ya kawaida haraka iwezekanavyo´´
Zaidi ya watu elfu nne wameachwa bila ya makazi wala mavazi baada ya nyumba na vitu vyao vyote kuchomwa na moto huo.
Ronny Macpherson ambaye alinusurika katika janga hilo amesema kuwa amebakiwa na nguo alizovaa tu pamoja na mbwa wake aliyemudu kukimbia naye.
Hapa tukimnukuu anasema
´´Nilikuwa nakwenda tu nakwenda hakuna kusimama, kama kulikuwa na kichaka chenye moto au mti nilipita, nikatoka pamoja na mbwa wangu´´mwisho wa kumnukuu
Mkazi mmoja Sam Gents alipiga kelele akiuliza kama kuna yoyote aliyemuona mkewe na wanawe watatu ambao walizingirwa na moto katika nyumba yao, yumkini waliteketea.
Miongoni mwa watu waliyouawa na moto huo ni mtangazaji wa mstaafu wa televisheni katika jimbo hilo, Brian Naylor pamoja na mkewe ambaye miaka 26 iliyopita aliripoti juu moto mkubwa uliyolikumba jimbo hilo na kuua watu 75.
Kwa mujibu wa msemaji wa polisi wa jimbo hilo la Victoria ambalo liko karibu na mji wa Melbourne ambao ni wa pili kwa ukubwa,Phil Shepherd watu waliyojaribu kukimbia kwa kutumia magari yao walikufa baada ya kuangukiwa na miti pamoja na kugongana na magari mengine kutokana na moshi.
CLIP: SHEPHERD 2
´´Wale ambao walifanikiwa kuingia katika magari yao kukimbia waliangukiwa na miti, magari mengine yalitumbikia katika mashimo na mengine yaligongana na baadaye wakazingirwa na moto´´
Baadhi ya waliyonusurika walikimbilia katika mabwawa ya kuongelea na kukaa ndani ya maji.
Dr De Villers Smit ambaye anawahudumia majeruhi anasema kuwa wengi wao asilimia 30 ya miili yao imeungua, ambapo baadhi wako katika hali mbaya zaidi ya wale waliungua katika shambulizi la bomu katika kisiwa cha Bali mwaka 2002.
Janga hilo la moto ni baya kabisa kwa janga la kiasili kuwahi kuikumba Australia katika kipindi cha miaka 110 iliyopita. Mwaka 1899 zaidi ya watu 400 waliuawa kutokana na kimbunga Mahina kilichoipiga Australia.
Mmoja wa manusura katika janga hilo Chris Harvey amekiambia kituo kimoja cha radio nchini humo ya kwamba hali ya jimbo hilo la Victoria itakuwa kama Hiroshima Japan ilipopigwa na bomu la atomik.