1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya Wanawake na Wasichana 200 wabakwa Sudan Kusini

Caro Robi
4 Desemba 2018

 Zaidi ya wanawake na wasichana 150 nchini Sudan Kusini wametafuta matibabu katika kipindi cha siku 12 zilizopita baada ya kubakwa na kufanyiwa unyanyasaji mwingine wa kingono. 

https://p.dw.com/p/39RJr
Süd Sudan UN Juba Flüchtlingslager
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Patinkin

Mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa, yametoa taarifa ya pamoja inayosema wanaume waliokuwa na silaha, wengi wao wakiwa wamevalia magwanda ya kijeshi waliwashambulia wanawake na wasichana katika mji wa kaskazini mwa Sudan Kusini wa Bentiu, jimboni Unity.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto, UNICEF, la kutoa misaada ya kiutu na lile la hazina ya idadi ya watu yamelaani mashambulizi hayo ya kinyama na kuwataka maafisa wa Sudan Kusini kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika na mashambulizi hayo.

Shirika la madaktari wasio na mipaka MSF wiki iliyopita lilisema wanawake na wasichana 125 walibakwa walipokuwa wakielekea katika vituo vya kutoa misaada ya chakula. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani mashambulizi hayo.

Afrika -Guinea Wurm
Wanawake na Watoto wa Sudan Kusini waathiriwa wakubwa wa mashambuliziPicha: picture-alliance/AP/M. Quesada

Umoja wa Mataifa walaani mashambulizi

Taarifa kutoka kwa katibu huyo imesema vitendo hivyo vya kutisha inakumbusha kuwa licha ya viongozi wa Sudan kusini katika kipindi cha hivi karibuni kuchukua hatua kujaribu kupunguza uhasama na kufikiwa kwa makubaliano ya amani, hali ya kiusalama nchini humo bado inasalia kuwa tete mno hasa kwa wanawake na watoto.

Guterres amezihimiza pande zote mbili zinazozana na viongozi wa siku za baadaye nchini humo kuhakikisha usalama wa raia na kushughulikia uvunjaji wa sheria bila kujali kwa kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanywa na waliohusika wanashitakiwa.

Naibu wa msemaji wa Guterres Farhan Haq amesema kikosi kimetumwa Bentiu na uchunguzi umeanzishwa.

Wanawake na watoto waathirika zaidi

Sudan Kusini ambayo imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2013, imeshuhudia viwango vya juu vya ghasia za kingono. Katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu, visa 2,300 vya ghasia za kingono vimeripotiwa, wengi wa waathiriwa wakiwa wanawake na watoto. Kulingana na Umoja wa Mataifa, asilimia 20 ya waathiriwa hao ni watoto.

Südsudan Rebellen
Wanajeshi wa Sudan KusiniPicha: Getty Images/AFP/C.A. Lomodong

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasema idadi kamili ya visa hivyo iko juu zaidi ya inavyoripotiwa kwasababu, matukio mengi hayaripotiwi. MSF imesema mbali na kubakwa, waathiriwa walicharazwa viboko, kupigwa kwa kitutuu ya bunduki na nguo, viatu na pesa zao kuibiwa na washambuliaji, zikiwemo kadi za kuwaruhusu kupokea misaada ya chakula.

Jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa mwezi uliopita waliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa kuna viwango vya kushtua vya ghasia za kingono na ukiukaji wa haki za binadamu Sudan Kusini. Baraza hilo la Usalama linatarajiwa kuujadili mzozo huo wa Sudan Kusini tarehe 18 mwezi huu.

Mkunga anayefanya kazi na MSF Ruth Okello anayewashughulikia wasichana na wanawake hao waliobakwa anasema hajawahi kushuhudia mashambulizi ya kinyama ya aina iliyoko Sudan Kusini ambako wanawake wazee, wajawazito na wasichana wa umri wa miaka 10 wakibakwa.

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Mohammed Khelef