1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya wanajeshi na polisi 150,000 kutumiwa

27 Mei 2014

Brazil itawatumia zaidi ya wanajeshi na polisi 150,000 ili kuimarisha ulinzi wakati wa dimba la Kombe la Dunia. Watapambana na maandamano ya kuipinga serikali yanayotarajiwa kufanyika wakati huo

https://p.dw.com/p/1C6bx
Brasilien / Soldat / Fußball-WM
Picha: picture-alliance/dpa

Maafisa wa Brazil wamesema kuwa kuwa wanajeshi 57,000 wataungana na polisi 100,000 na maafisa wengine wa usalama kuvilinda viwanja 12 vitakavyoandaa mechi za dimba la Kombe la Dunia, pamoja na mahoteli na viwanja vya ndege.

Waziri wa ulinzi Celso Amorim anasema Brazil “imejiandaa vilivyo” kuhakikisha usalama wa wakaazi na mamia kwa maelfu ya wageni wanataotarajiwa kusafiri nchini humo wakati wa tamasha hilo maarufu.

Maafisa wamesema gharama ya hatua za ziada za usalama ni euro milioni 628, kitu ambacho hakitawafurahisha Wabrazil wengi, ambao wanahoji kuwa badala ya kutumia mamilioni katika kuandaa Kombe la Dunia, serikali inastahili kuwekeza fedha hizo katika mambo kama vile huduma za afya, elimu na usafiri.

Brasilien Recife Streik der Polizei Plünderungen 15.05.2014
Maduka yaliporwa wakati wa mgomo wa polisi kudai nyongeza ya mishahara na mazingira bora ya kaziPicha: Reuters

Takribani watu milioni moja waliingia barabarani wakati wa kinyang'anyiro cha Kombe la Mabara mwaka jana, katika maandamano ambayo wakati mwingine yaligeuka kuwa ghasia. Rais Dilma Rousseff kisha akatoa hotuba kwenye televisheni na kuahidi kuyashughulikia matakwa ya waandamanaji.

Hata hivyo Waziri wa Sheria Jose Eduardo Cardozo anasema hatarajii maandamano ya Kombe la Dunia kuwa makubwa kama yale ya mwaka jana. Hata hivyo maandamano yameendelea kushuhudiwa nchini humo huku kukiwa na migomo kadhaa, ambapo polisi, walimu, na madereva wa mabasi wakishiriki migomo kabla ya kuanza Kombe la Dunia.

Cardozo amesema maandamano ya amani yataruhusiwa wakati wa kinyang'anyiro hicho, lakini maafisa wa usalama watajiandaa kupambana na matatizo yoyote, hasa kama maandamano hayo yatatishia kuvuruga michezo itakayokuwa ikiendelea.

Waziri wa Ulinzi Amorim anasema kama wanajeshi wan chi hiyo watalazimika kuchukua hatua, kwanza watatumia mbinu zisizo hatari.

Mwandishi: Bruce Amani/ Reuters, AFP, AP, dpa
Mhariri: Mohammed Dahman