Zaidi ya wanajeshi 30 wauwawa na wanamgambo Nigeria
26 Aprili 2021Mashambulizi hayo yanatajwa kufanywa na wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu katika kanda ya Afrika Magharibi, ISWAP. Siku ya Jumapili mchana, wapiganaji wa kikundi hicho waliivamia kambi ya jeshi mjini Mainok katika jimbo la Borno lililopo kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuwaua wanajeshi zaidi ya 30.
Walioshuhudia tukio hilo waliliambia shirika la habari la Reuters kwamba wapiganaji hao walikuja katika eneo hilo wakiwa wamevalia kama wanajeshi na kwa kutumia malori takribani 16 yenye bunduki na magari mengine 6 ya kijeshi. Mmoja wa wanajeshi aliyeshuhudia hayo alisema.
soma zaidi:Utekaji Nigeria wafikia kiwango cha mzozo
Baada ya muda wa saa chache wapiganaji hao walifanikiwa kuiteka kambi nzima na hapo ilibidi wanajeshi waite ndege za mashambulizi ya angani. Kwa mujibu wa mwanajeshi huo, wanajeshi wengi waliuawa pale mashambulizi ya anga yalipoanza. Mmoja wa wakazi wa eneo hilo alisema kwamba washambuliaji hao pia walichoma makao makuu ya polisi ya mji huo.
Mkazi wa eneo hilo, Ba Umar Abba Tuja ni kati ya watu walioshuhudia mashambulizi hayo na aliimbia Reuters na hapa namnukuu, ''ndege za mashambulizi ya angani zilipoanza kurusha mabomu kutoka hewani, wapiganaji walikimbilia vijijini na kujificha katika shule ya msingi,'' mwisho wa kumnukuu. Tuja aliongeza kwamba wapiganaji wa kikundi cha kigaidi waliondoka usiku wa manane.
Usalama bado sio shwari Nigeria
Mji wa Mainok upo umbali wa kilomita 55 kutoka mji wa Maiduguri, ambao ndio mji mkuu wa jimbo la Borno. Makundi ya kigaidi yenye itikadi kali za Kiislam yamekuwa yakiliathiri eneo hilo la kaskazini mashariki mwa Nigeria kwa zaidi ya muongo mmoja sasa. Mpaka sasa makundi hayo yamewaua watu zaidi ya 30,000 na kusababisha watu takribani milioni 2 kupoteza makazi yao.
soma zaidi:Maelfu wakimbia mashambulizi ya wabeba silaha Nigeria
Ukosefu wa usalama nchini Nigeria kwa mwaka huu pekee umesababisha wanajeshi na raia kadhaa kuuawa. Ni zaidi ya mwezi mmoja tu ambapo wanajeshi 30 waliuwawa katika mashambulizi manne tofauti yaliyofanywa na wanamgambo hao wa Kiislamu wa kaskazi mashariki mwa Nigeria.
Kikundi hicho cha ISWAP kilijitenga na kikundi cha Boko Haram miaka michache iliyopita na sasa kimeanzisha mashambulizi yake binafsi dhidi ya wanajeshi na raia katika eneo hilo.
Chanzo: rtre/afpe